Mavunde aagiza kampuni kutozwa faini ya Sh1.4 milioni

Tuesday October 22 2019

 

By Beldina Nyakeke, Mwananchi [email protected]

Serengeti. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu nchini Tanzania, Anthony Mavunde ameitaka kampuni ya Grumeti Reserve kulipa faini ya Sh1.4 milioni baada ya kubainika wafanyakazi wake kufanya  shughuli zao bila kuvaa mavazi ya usalama kazini.

Mavunde ameigiza Mamlaka ya Usalama Mahala pa Kazi (Osha)  kuhakikisha wanachukua faini hiyo ya Sh1.4 milioni kwa kampuni hiyo inayojishughulisha na masuala mbalimbali, yakiwemo ya utalii katika mapori ya akiba  kijiji cha Makundusi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 22, 2019 baada ya kuitembelea kampuni hiyo,  Mavunde amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi ni wajibu wa mwajiri kuhakikisha  wafanyakazi wake wanafanya kazi katika mazingira salama.

Mavunde amesema katika ziara hiyo amegundua zaidi ya wafanyakazi 25 wa kitengo cha ujenzi na ufundi wanafanya kazi bila kuwa na vifaa hivyo na baadhi wakiwa wamefanya kazi katika hali hiyo kwa miaka mitano.

“Nimekaa saa moja tu hapa lakini nasikia vumbi limejaa kifuani, sasa hawa watu wamefanya kazi hapa wengine hata miaka minane bila kuwa na vizuia vumbi wala mabuti,  hivi hii ni haki kweli,” amehoji Mavunde.

Mbali na kuwataka kulipa faini, Mavunde ametoa muda wa siku saba kwa kampuni hiyo kuhakikisha vifaa vya kazi vinapatikana na wafanyakazi wote wanapatiwa.

Advertisement

Ofisa rasilimali watu wa kampuni hiyo, Martha Baare amesema kampuni hiyo imeagiza vifaa hivyo nchini Afrika Kusini.

Amesema walipobaini kutokuwepo kwa vifaa hivyo  walitoa taarifa kitengo cha utawala Agosti, 2019, kwamba muda wowote watapokea vifaa hivyo.

Advertisement