Mawakili wakwamisha kesi ya Mbowe, wenzake

Tuesday September 17 2019

 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutokana na mawakili wa utetezi kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.

Kesi hiyo namba 112/2018 ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi.

Wakili Gaston Garubindi amedai hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019  akieleza kuwa maelekezo aliyopewa na wakili Peter Kibatala anaomba shauri hilo liahirishwe hadi Oktoba 7, 2019.

"Wakili Profesa Safari (Abdallah) yuko Mahakama Kuu Shinyanga mbele ya Jaji Mkeha na Kibatala yuko Mahakama Kuu mbele ya Jaji Tiganga baada  ya kupata wito wa dharura jana kutakiwa afike mahakamani hapo leo,” amedai wakili Garubindi.

Wakili Garubindi amedai wakili mwingine katika kesi hiyo, Hekima Mwasipu yuko Mahakama Kuu Tanga kwenye kesi ya madai namba 7/2019 mbele ya Jaji Mruma.

Sababu nyingine iliyoelezwa na wakili Garubindi ni mshtakiwa wa pili, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji  Peter Msigwa na mshtakiwa wa nane, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche wamefiwa na ndugu zao hivyo wanafanya taratibu za kwenda kwenye mazishi.

Advertisement

"Kwa kuwa mawakili wote wapo Mahakama Kuu  wamesababisha tuombe kuahirishwa kwa kesi hii na kuomba ipangwe Oktoba 7 au 10,” amedai.

Wakili mkuu wa Serikali, Faraji Nchimbi alipinga sababu hizo kutokana na kutoelezwa Profesa Safari yupo katika kesi gani, sambamba na barua ya wito.

" Kesi hii inawakilishwa na jopo la mawakili akiwemo Jeremia Mtobesya, John Mallya na Dickson Matata wote hawa hawapo na haijaelezwa mahakama wako wapi,” amedai Nchimbi.

Kuhusu Mchungaji Msigwa na Heche kusafiri, amesema kuna haja ya kusikia kutoka kwa washtakiwa wenyewe pamoja na kupata uthibitisho ikiwemo cheti kwa ajili ya kumbukumbu ya mahakama.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alieleza kutoridhishwa kuahirisha kesi hiyo kwa siku 20 na kuipanga kuendelea Septemba 24 hadi 27 na Oktoba 1 hadi 3, 2019.

Washtakiwa wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Mbowe na viongozi wengine wanakabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, ikiwemo kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa,na kufanya mkusanyiko usio halali

 

Advertisement