Mawakili wataja mazuri na dosari uongozi wa Magufuli

Wednesday November 6 2019

 

By Daniel Mjema, Mwananchi

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli zilipitishwa sheria mbalimbali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kusaidia Serikali kutimiza majukumu yake.

Sheria takriban 20 zilitungwa na kupitishwa na Bunge tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015.

Licha ya kuwepo kwa sheria nyingi, sheria tano ndio ambazo zilizua gumzo na hisia tofauti miongoni mwa wadau nchini.

Sheria zilizozua mjadala zaidi ni lle ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, ambayo ndio ya kwanza kupitishwa na uongozi wa Rais Magufuli.

Sheria nyingine ni pamoja na ile ya Madini, Mafuta na Gesi ya mwaka 2017, Vyama vya Siasa (2019) na marekebisho ya Sheria ya Takwimu yaliyofanywa mwaka jana.

Pia kuna marekebisho ya sheria yanayohusu vyama visivyokuwa vya kiserikali (NGO’s).

Advertisement

Wanasheria mbalimbali nchini wamechambua miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli huku wengine wakikosoa baadhi ya sheria alizozisaini ingawa zilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wameainisha mambo sita mazuri na yale yenye walakini katika utendaji wake tangu alipochaguliwa.

Mambo hayo yamejikita katika suala la utawala bora, sheria mbalimbali, vita dhidi ya rushwa na ufisadi na ujenzi wa miundombinu.

Mambo mazuri ya JPM

Frank Mushi, wakili anayeishi jijini Dar es Salaam anasema tangu Rais Magufuli aingie madarakani, zipo sheria mbalimbali ambazo amezisaini ambazo ni nzuri na ambazo si nzuri.

“Mfano, sheria za usimamizi wa madini zilizopitishwa chini ya utawala wake ni nzuri zinazolenga kusimamia rasilimali madini katika mapana yake,” anasema Mushi.

“Sheria hizi zimesaidia kumilikisha moja kwa moja rasilimali madini kwa nchi na kuweka mamlaka ya usimamizi wake katika mikono ya nchi. Huko nyuma sekta hii ilichezewa sana kwa sababu ya ubovu wa sheria.

“Lakini, `Media Services Act 2016’ (Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari) kwa kiasi fulani imesaidia sana namna ya kudhibiti ukanjanja katika tasnia hiyo ingawa utekelezaji wake pia umeminya uhuru wa habari,” anasema Wakili Mushi.

Mushi alipongeza mapendekezo ya marekebisho kwenye Sheria ya Mwenendo wa Jinai ambapo sasa kumeingizwa kipengele cha kujadiliana kukiri kosa (plea bargaining).

“Hii imetumiwa kwa miaka mingi huko Ulaya na Marekani. Kwetu ndio imeanza japo kuanza kwake kumekuwa na dosari za kiutekelezaji, mathalani kuwekwa kwa ukomo wa kuomba ku-`bargain’ (kujadiliana),” anaongeza Mushi.

Wakili huyo pia alisifia miaka minne ya utawala wa Magufuli kwa kufanya mapinduzi makubwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu.

“Tunaona barabara zinajengwa kila kona na vituo vya mabasi. Bila kusahau ujenzi wa madarasa na vituo vya afya na ndege zinanunuliwa na huku ujenzi wa reli ya kisasa ukiendelea. Katika maeneo hayo amefanya vizuri,” anaeleza Wakili Mushi.

Aliongeza pia uongozi wa Magufuli umesaidia kupunguza tatizo la rushwa na hasa katika sekta ya umma.

Naye mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS) tawi la Kilimanjaro, David Shillatu anafafanua namna sheria tatu za Bunge za mwaka 2017 zilivyoweka msingi mzuri katika usimamizi wa rasilimali za madini.

“Kimsingi sheria hizi zilileta mabadiliko makubwa ya namna ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini nchini, ni jambo Magufuli anapaswa kupewa sifa,” anasema Shillatu.

Wakili Peter Mshikilwa wa jijini Dar es Salaam anasema kwa miaka minne ya utawala wake, Magufuli amerudisha nidhamu ya utumishi wa umma.

“Amejitahidi kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa kodi na ametekeleza miradi mikubwa katika kipindi kifupi sana. Kiujumla amejitahidi,” anaeleza Mshikilwa.

Mshikilwa alisifia sheria ya madini ingawa alitaja changamoto kwenye suala la kuchakata madini.

“Sheria inataka tuchakate madini yetu hapahapa, lakini hili linawawia vigumu wawekezaji kwa sababu linahitaji uwekezaji mkubwa. Hili naamini mwaka mmoja huu uliobaki atalishughulikia,” anasema Mushi.

Dosari za uongozi wake

Wakizungumzia dosari za utawala wa Magufuli, Wakili Mushi anataja baadhi ya sheria ambazo Rais alizisaini na ambazo zinaleta ukakasi kuwa ni Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

“Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari inagusa uhuru wa kupata habari ambao uko `guaranteed’ (umehalalishwa) kwenye Katiba,” anaongeza Mushi.

“Hii ni moja ya sheria tunayoweza kusema sio nzuri kwa baadhi ya vifungu hasa vinavyoweka urasimu katika upatikanaji wa taarifa. Media Service Act ya 2016 nayo ni sheria yenye mapungufu mengi.

“Mfano, kifungu cha 53(2) cha hiyo sheria kinasema ukikutwa na andiko au gazeti lenye maneno ya uchochezi bila sababu ya msingi unapigwa faini au kifungo. Hapa kuna shida.

“Pia kuna marekebisho ya Sheria ya Takwimu nayo yalileta mkanganyiko. Katika miaka minne kumekuwa na kurudi nyuma kwa kiasi fulani kwenye utendaji kazi wa mahakama.

“Katika mashauri ya jinai hasa yanayohusu wanasiasa kumekuwa na malalamiko mengi. Kuna watu bado wana wasiwasi na uhuru wa mahakama,” alisema Mushi.

Naye Wakili Shillatu anasema pamoja na mazuri mengi ya Rais Magufuli, lakini Sheria ya Vyama vya Siasa iliyorekebishwa imekua ni sheria iliyotia doa katika utawala wake.

“Pengine ingekuwa jambo zuri sana kwa utawala huu kuruhusu kupanuka kwa demokrasia katika nyakati hizi ambazo kauli mbiu ya serikali ni Ukweli na Uwajibikaji,” anasema Shillatu.

“Serikali ingefanya jambo kubwa kama ingeruhusu kwa uwazi kabisa kazi za vyama vya siasa, hivyo kukuza demokrasia. Hii kuzuia jambo la kikatiba na kisheria kumetia doa,” anasema.

Kama walivyo wanasheria wengine, Wakili Mshikilwa anasema sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari ya 2016 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2019, zinatia doa mazuri mengi ya Rais Magufuli.

Tundu Lissu alia Utawala Bora

Tundu Lissu, mwanasheria mkuu wa Chadema, ambaye bado yupo nje ya nchi baada ya kukamilisha matibabu anasema baadhi ya sheria zilizotungwa na Bunge na kusainiwa na Rais Magufuli sio nzuri.

“Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali yametengeneza utaratibu kwa vyama vya siasa vya upinzani na asasi za kiraia kuwa mgumu,” alisema.

“Ni (utaratibu) mgumu na unatishia uhai wa vyama na mashirika hayo. Sheria hizi zimefuta mazuri karibu yote yaliyoletwa na Hati ya Haki za Binadamu mwaka 1984 na mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Lissu anasema Tume ya Nyalali ilipendekeza kufutwa au kurekebishwa kwa Sheria Kandamizi 40, lakini badala ya kuzipunguza au kuziondoa, utawala wa sasa umeziongeza sheria hizo kandamizi.

Lissu amedai baadhi ya sheria ni zile zinazotishia uhuru wa vyombo vya habari na kudai kuwa utawala wa miaka minne wa Magufuli umerudisha Tanzania likija suala la demokrasia.

“Serikali imetunga au kutilia nguvu sheria mbalimbali ambazo kwa ujumla zimeathiri uhuru wa vyombo vya habari na wa taaluma nzima ya habari. Unahatarisha uhuru wa vyombo vya habari.

“Kuhusu demokrasia, utawala wa Rais Magufuli umebana mfumo wa demokrasia wa vyama vingi vya siasa nchini,” anasema Lissu.

“Utawala wake umehalalisha matumizi ya nguvu za dola dhidi ya vyama vya upinzani. Utawala wake umeleta siasa mpya Tanzania,” amesema Lissu.

Advertisement