Mawaziri sita wasioshikika Awamu ya Tano

Dar es Salaam. Ni zaidi ya miaka minne sasa tangu Rais John Magufuli aunde baraza lake la kwanza la mawaziri lililotawaliwa na kuteua na kutengua na baadhi kuhamishwa, lakini ni mawaziri sita tu ambao hawajaguswa na misukosuko hiyo.

Kati ya hao, wawili waliwahi kukosolewa hadharani, lakini pengine ni kutokana na utendaji wao au kujirekebisha, hawakuondolewa na kuna uwezekano wakamaliza miaka mitano kwa amani, licha ya Rais kusema ataendelea kutengua na kuteua hadi wasaidizi wake wamuelewe.

William Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi), Ummy Mwalimu (Afya), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango) na Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge) ndio ambao hawajaguswa na misukosuko hiyo tangu Rais Magufuli aunde baraza la kwanza.

Alitangaza awamu ya kwanza Desemba 10, 2015 ikiwa na upungufu wa nafasi nne ambazo ni za Waziri wa Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Elimu.

Nafasi hizo alizijaza wiki mbili baadaye.

Pamoja na kusema kuwa katika utawala wake hataacha kubadilisha mawaziri hata ikiwezekana wabunge wote wa Bunge la Jamhuri waonje nafasi hizo kama waliopo hawatajirekebisha, bado makada hao sita hawajapata misukosuko.

Juhudi za kuwapata mawaziri hao kuzungumzia siri ya kutokumbwa na misukosuko hiyo hazikufanikiwa, hata walipotumiwa ujumbe wa maandishi, hawakujibu.

Lakini wengi waliondolewa kutokana na kashfa zilizozikumba wizara zao, kutowajibika ipasavyo katika matukio kama ajali, kutoonyesha tabia njema hadharani na wengine waliondolewa kimyakimya.

Rais pia ana utamaduni wa kuweka bayana makosa ya mawaziri wake kila anapotengua, kama ilivyotokewa kwa January Makamba, Mwigulu Nchemba, Profesa Sospeter Muhongo na Kangi Lugola.

“Kinachotokea hivi sasa ni kwamba Rais hataki utani, wala hatanii na anahitaji uwajibikaji na asiyeweza anamuondoa,” alisema Jaffary Ally, kada wa CCM ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

“Nafikiri huko nyuma kulikuwa na uzembe mwingi wa viongozi na kutowajibika, hivyo watu walishajenga mazoea. Yatafanyika makosa kwenye eneo lake anajua atahamishiwa eneo jingine.”

Mabadiliko yaliyofanywa mwisho wa wiki iliyopita ya kumuondoa Lugola Wizara ya Mambo ya Ndani yamefanya mawaziri walioondolewa katika Baraza la Mawazi tangu alipomtimua waziri wa kwanza Charles Kitwanga, kufikia 12 na manaibu 13. Rais aliunda baraza la kwanza lililokuwa na wizara 18 na mawaziri 19.

Lugola aliondolewa kutokana na wizara yake kuingia mkataba ambao Rais ameuita “wa hovyo” wa ununuzi wa vifaa vya uokoaji.

Walivyoanza kutenguliwa

Waziri wa kwanza kuonja anguko kutoka barazani ni Kitwanga aliyekuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ambaye Mei 21, 2016 alienguliwa kwa madai ya kuingia bungeni akiwa amelewa.

Kitwanga, ambaye ni mbunge wa Misungwi (CCM) alirithiwa na Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambayo baadaye ilitenganishwa na kuwa wizara mbili za Kilimo na nyingine ya Mifugo na Uvuvi.

Julai Mosi mwaka jana, Dk Mwigulu, ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) naye alijikuta akiondoshwa kwenye wizara hiyo na nafasi yake kuteuliwa Kangi Lugola aliyekuwa naibu waziri ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira).

Wizara nyingine ambayo imefanyiwa mabadiliko mara kadhaa ni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambapo Novemba 10, 2018 Rais Magufuli alimteua Joseph Kakunda kuwa waziri wa wizara hiyo ambayo kabla ilikuwa ikishikiliwa na Charles Mwijage.

Hata hivyo, Kakunda, ambaye ni mbunge wa Sikonge (CCM) hakumaliza hata mwaka katika wizara hiyo, kwani Juni 8, 2019 aling’olewa na nafasi yake kuchukuliwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa aliyepo madarakani mpaka sasa.

Wizara ya Kilimo pia imefanyiwa mabadiliko mara tatu ikianza na Dk Mwigulu Nchemba ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Baada ya Dk Mwigulu kuhamishwa ilishikwa na Dk Charles Tizeba aliyesombwa na mzozo wa korosho kabla ya kuteuliwa Japhet Hasunga kushika wizara hiyo.

Waziri mwingine aliyepoteza nafasi yake mapema tu ni Nape Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari, UtamadUni, Sanaa na Michezo, yeye aliyetenguliwa Machi 23, 2017.

Nape aliondolewa wakati akiwa ameunda kamati ya kufuatilia tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kudaiwa kuvamia studio za Clouds Media Group zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na kudaiwa kulazimisha kurushwa kwa kipindi kinyume na taratibu za kampuni hiyo.

Pengine waziri aliyekaa muda mrefu bila kuguswa alikuwa January Makamba aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), lakini ilipofika Julai 21, 2019 naye alisombwa baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza lake na kumteua tena George Simbachawene kushika wizara hiyo.

Makamba ni miongoni mwa wabunge vijana wa CCM waliotajwa kumwomba msamaha Rais Magufuli kwa utovu wa maadili mwishoni mwa mwaka jana. Wengine ni Nape Nnauye (Mtama) na William Ngeleja (Sengerema).

Waziri mwingine aliyepoteza nafasi yake alikuwa Gerson Lwenge ambaye baadaye uteuzi wake ulitenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Issack Kamwelwe.

Awali, Wizara hiyo iliongozwa na Profesa Makame Mbarawa ambaye kwa sasa ni Waziri wa Maji.

Mawaziri wengine walibadilisha tu wizara wakiwemo Dk Augustine Mahiga aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria, huku aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Profesa Palamagamba Kabudi kuchukua mikoba ya Dk Mahiga baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko madogo Machi 3, 2019.

Mbali na mawaziri hao kuondolewa, Waziri anayeonekana kuwa na bahati ni George Simbachawene aliyeingia na kutoka katika Wizara tofauti tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani.

Awali Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, lakini alitangaza kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya madini ya almasi na Tanzanite Septemba 2017.

Lakini Simbachawene alirudishwa katika Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) baada ya kuenguliwa kwa Makamba. Wiki iliyopita amemrithi tena Lugola aliyekuwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Wizara zaongezeka

Awali Rais Magufuli aliunda Wizara 18 lakini baadaye ziliongezeka baada ya kuigawanya Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora na kumteua George Mkuchika kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku pia akimpandisha Selemani Jafo kuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais, Tamisemi.

Wizara nyingine iliyogawanywa ni ya Kilimo na Mifugo, ambapo alimteua Luhaga Mpina kuwa Waziri wa Mifugo, huku akimteua Charles Tizeba kuwa Waziri wa Kilimo. Hata hivyo kwa sasa wizara hiyo inaongozwa na Japhet Hasunga.

Nyingine ni iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini ambapo Rais Magufuli alimteua Merdard Kalemani kuwa Waziri wa Nishati huku Wizara ya Madini akimteua Angela Kairuki, lakini baadaye alimhamishia katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa Waziri anayesimamia Uwekezaji na nafasi yake kushikiliwa na Doto Biteko.