Mawaziri wa mambo ya Nje, Ulinzi wa Sadc wakutana Tanzania kuijadili DRC Kongo

Muktasari:

Hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imewakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje pamoja na mawaziri wa ulinzi na vyombo vya ulinzi  vya Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (Sadc) ijulikanao kama ‘Double Troika’ ambao watajadili na kutoka na hatua za kuchukuliwa ili kurejesha amani.

Dar es Salaam. Mawaziri wa Mambo ya Nje pamoja na mawaziri wa ulinzi na vyombo vya ulinzi  vya Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (Sadc) ijulikanao kama ‘Double Troika’ wamekutana kwa dharura kujadili hali ya kisasa na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha amani katika nchi hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa dharura wa Double Troika inayojumuisha Troika ya siasa na Troika ya Ulinzi na Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje  wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema lengo la mkutano huo wa dharura ni kuweka mikakati itakayosaidia kuimarisha amani nchini DRC na kumaliza migogoro inayotishia ustawi wa nchi hiyo iliyodumu kwa miongo mingi.

Aidha, Waziri Kabudi amebainisha  mkutano huo utasaidia nchi za Sadc zenye vikosi vya ulinzi na usalama nchini DRC yaani Tanzania, Malawai na Afrika Kusini kuimarisha amani na DRC kwa kufanya tathmini na kukubaliana hatua za kuchukua ili vita na migogoro ya mara kwa mara inayoibuka nchini hiyo ifikie tamati na amani ya kudumu ipatikane.

“Mkutano huu wa leo ni wa Troika ya Siasa na Troika ya ulinzi na usalama ambapo kupitia mkutano huu tunaamini kuwa tutafanya tathimini ya hali ya amani DRC na kukubaliana ni hatua gani za kuchukua,” amesema Profesa Kabudi

Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi ameongeza ndani ya mwaka 2019 amani na demokrasia vimezidi kuimarika katika nchi wanachama wa Sadc, kutokana na baadhi ya nchi wanachama kuendesha chaguzi za kidemokrasia zilizomalizika kwa amani katika nchi za Msumbiji na Botswana. 

Profesa Kabudi amesema Tanzania na nchi 16 wanachama wa Sadc bado zinaendelea kupaza sauti kwa jumuiya za kimataifa na nchi ambazo zimeiwekea vikwazo Zimbabwe kuviondoa mara moja kutokana na vikwazo hivyo kutokuwa na uhalali jambo linalosababisha mateso kwa raia wa nchi hiyo hususani akina mama na watoto .

"Katika hili la Zimbabwe lazima sisi kama Sadc tushikamane na kusafiri pamoja ili tufike kwa umoja wetu," amesema Profesa Kabudi.

Awali, akitoa hutuba katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Sadc, Dk Stegomena Taxi amesema ana matumaini makubwa na mkutano huo unaofanyika jijini Dar es salaam utatathimini na kutoa mapendekezo ya muda mfupi na mrefu kuhusu hali ya usalama, amani na siasa katika nchi ya DRC  na ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ili kuhakikisha ukanda huo unakuwa salama na amani

Ameongeza amani na usalama ni nyenzo mojawapo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na hivyo kupata maendeleo yanayohitajika kwa ajili ya mataifa ya Afrika.