Mazungumzo Kulthum Mansoor wa Takukuru, DDP yagonga ukuta

Muktasari:

Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Takukuru, Kulthum Mansoor umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendelea na shauri hilo kwa kuwa mazungumzo yao na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) hayakufikia muafaka.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Takukuru, Kulthum Mansoor umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendelea na shauri hilo kwa kuwa mazungumzo yao na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) hayakufikia muafaka.

Oktoba 2, 2019 wakili wa utetezi, Elia Mwingira aliieleza mahakama hiyo kuwa wameandika barua kwa DPP kuomba msamaha na kukiri makosa yanayomkabili Kulthum.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 12, 2019 baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon kudai mbele ya Hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina  kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo, Mwingira amedai  Oktoba 30, 2019 walienda kwa DPP lakini walipozungumza naye hawakufikia muafaka, kuomba mahakama hiyo kuendelea na kesi hiyo.

"Kwa DPP tuliona mazungumzo hayana mwelekeo tunaomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi kwa kuwa mshtakiwa yupo ndani kwa muda mrefu," amedai Mwingira.

Hakimu Mhina amesema upande wa mashtaka wahakikishe upelelezi unakamilika na kuahirisha shauri hilo hadi Novemba 26, 2019.

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya  Agosti  13, 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya  ya Bagamoyo huku akijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la pili, inadaiwa  kati ya Januari 2012 na Mei 2017  huko maeneo ya Upanga ndani ya Wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa kudanganya, alijipatia Sh5.2 milioni  kutoka kwa Alex Mavika ambaye ni mfanyakazi wa Takukuru, kama malipo ya kiwanja  kilichopo Kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Pia, inadaiwa kati ya tarehe hizo,  Mansoor alijipatia Sh3 milioni kutoka kwa Wakati Katondo kama malipo ya kiwanja kilichopo maeneo ya Kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kuwa  alijipatia Sh5milioni  kutoka kwa Ofisa wa Takukuru, Gogo Migutah kama malipo ya kiwanja kilichopo eneo hilo.

Katika shtaka la tano, inadaiwa Mansoor alijipatia Sh7 milioni kutoka kwa Ekwabi Majungu  ambaye pia ni ofisa wa Takukuru kama malipo ya kiwanja hicho.

Mansoor anadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017, maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa ofisi hiyo, alijipatia Sh7 milioni kutoka kwa John Sangwa kama malipo ya kiwanja cha eneo hilo.

Indaiwa kuwa mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru, alijipatia Sh5 milioni  kutoka kwa Rose Shingela kwa ajili ya malipo hayo.

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha,  inadaiwa kati ya Januari 2013 na Mei 2018 huko maeneo ya Upanga, mshtakiwa  alijipatia Sh1,477,243,000 wakati akijua kuwa  fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa tangulizi la kughushi.