Profesa Mbennah, balozi mpya Zimbabwe aliyeanza kuvaa viatu akiwa darasa la saba

“Nilipata Uteuzi nikiwa ndani ya teksi nikielekea kupanda ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, nilihisi ni ndoto na nilijiuliza maswali mengi, why me? (kwanini mimi),” ni maneno ya Profesa Emmanuel Mbennah, balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Profesa Mbenah ni miongoni mwa mabalozi wanne walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais John Magufuli, kwenda kuiwakilisha Tanzania nchi za nje na yeye amepelekwa Zimbabwe.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, Profesa Mbennah anasema alipata simu ya kwanza kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa amepokea ujumbe mbalimbali wa simu ukimpongeza kwa uteuzi lakini hawakuwa wamesema uteuzi gani.

Mbennah anasema katika maisha yake hakuwahi kuwaza kama angeshika nafasi ya ubalozi, lakini hakuweza kukataa uteuzi huo kwa kuwa kazi aliyopewa ni ya heshima ambayo inampasa kutumia elimu yake kwa faida ya Watanzania.

Kazi ya ubalozi

Akizungumza kuhusu jukumu hilo jipya alilopewa na mkuu wa nchi, anasema si kazi lelemama na wala hapaswi kujisifu kwa kazi hiyo, bali anapaswa kumtanguliza Mungu ili atimize matakwa ya aliyemteua na ya Watanzania kwa ujumla.

“Ninakwenda Zimbabwe nchi ambayo haijatulia, watu wanahitaji mamilioni kwa ajili ya kununua mkate wa siku, siasa zake hazijatulia, uchumi wake hauko vizuri, lakini ninakwenda kifua mbele bila woga wala hofu nikijua kuna kitu moyoni mwangu cha kufanya,” alisema.

Balozi huyo anasema, kazi atakayoanza nayo ni kutengeneza umoja na mabalozi wengine ili kusaidia nchi ya Zimbabwe iondolewe vikwazo vya kiuchumi, jambo alilosema likiondolewa, hata wananchi wake watatulia na kuanza kutafuta maisha mengine ndani ya nchi yao.

Anataja kitakachomsaidia katika kufanikisha hayo kuwa ni kutumia weledi, imani, mahusiano mazuri na nchi myingine na kufanya kazi bila ulegevu wakati wote kutafuta fursa za Watanzania kwa taifa hilo.

Hata hivyo, Profesa Mbennah anasema kazi ya Balozi ni ngumu na kwa upande mwingine ni nyepesi, akitaja ugumu pale anapojihusisha na watu wengi kwa wakati mmoja ambao anatakiwa kutambua mahitaji yao nyakati zote.

Kuhusu wepesi anasema ni pale mtu anapohitaji kujifunza kutoka kwa wengine na kusikiliza wengine huku akijivunia kuijua historia ya nchi yake na mahusiano yake kwa nchi anayokwenda, kitu ambacho anasema kitakuwa kigezo chake katika uwakilishi.

“Hayo yote nitayafanya nikimtanguliza Mungu mbele,. Nitatanguliza maslahi ya Watanzania, nitatunza heshima aliyonipa Rais kwani ana wasomi wengi lakini kwa nini mimi, kwa hakika ninalo deni kubwa kwa wananchi na serikali yangu. Naomba mniombee,” anasema Profesa Mbennah na kuongeza

“…nayaona maono ya kiongozi wa nchi yangu, nitayaishi, lakini na mimi nina maono makubwa kwa nchi yangu, nitayatumia na kwa kweli hakuna kitakachoshindikana kwa kila hatua, kikubwa ni kujishusha na kutotaka nijiinue.”

Alipotakiwa kujibu kuhusu hali ya Zimbabwe na siasa zake, alisema anatambua tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo, Marehemu Robert Mugabe hakujawa na utulivu wa kutosha, kwa hiyo kazi atakayofanya ni kupeleka heshima ya Tanzania kama ilivyo historia katika upatanishi na angetamani kuona Wazimbabwe wakiwa kitu kimoja kwa kutumia diplomasia yake.

Mbenah ambaye pia ni mchungaji, anasema katika mambo yote Mungu akiwa mbele hakuna jambo litakalokosa majibu hata kama lingekuwa namna gani.

Fursa za Watanzania Zimbabwe

Anasema kwa sasa hawezi kuzitaja fursa zilizopo, lakini kwa mazingira yake hana wasiwasi kutokana na kazi aliyoifanya kwa muda mrefu katika utafiti wa mataifa yaliyokuwa na machafuko na vita Afrika.

Kwa mujibu wa Profesa huyo, hata zile zinazotajwa kuwa ni changamoto, kwake angetamani zigeuzwe kuwa fursa hivyo hawezi kuwa na maneno ya kusema kwa sasa angetaka nini, bali atafungua milango kwa Watanzania kukutana naye na atawaeleza wafanye nini kwa wakati gani ili kunufaika na uwepo wake.

Huku akisema asingependa kuwa mwanasiasa na hasa katika kugombea nafasi za ubunge, anasema diplomasia itachukua mkondo wake katika kuwasemea wanyonge na wenye mahitaji, lakini rasilimali za Tanzania zitalindwa na nchi itanufaika kupitia kwake.

Pamoja na kuwa hakuomba kazi ya ubalozi, bado anaona uwezo na ari ya kufanya kazi hiyo anayo kwani tangu siku ya uteuzi amekuwa akitafakari na kuona anao mzigo na angetamani kutengeneza historia iliyotukuka.

Anachotamani

Balosi huyo ambaye pia ni kiongozi wa kiroho anaondoka Tanzania akitamani siku akirudi akute sheria ya mtoto ikiwa imeweka usawa na mkakati wa kuwalinda watoto kwa wanaopata mateso ambao wanaitwa “watoto wa mitaani”.

Katika kusisitiza hilo anapinga kauli za wanasiasa kuwa ‘mtoto ni taifa la kesho’ akisema kauli hiyo inapotosha kwani mtoto ni taifa la leo bali ni kiongozi wa kesho.

“Natamani kama ipo haja tubadili sheria ili kulinda kikamilifu makundi ya watoto wote na hasa waliopo kwenye mazingira magumu. Ikitokea namna hiyo nitamshukuru Mungu kuwa tumefanikiwa,” anasema Mbennah.

Uzoefu wa miaka saba akifanya kazi kama mkurugenzi wa Compassion anasema ulimpa nafasi ya kuwatambua watoto na kuyaishi maisha yao.

Anatolea mfano alikotoka yeye, akisema alivaa viatu kwa mara ya kwanza akiwa darasa la saba mwaka 1976 na viatu vyenyewe vilinunuliwa kwa mchango wa walimu wake, hivyo aliishi katika mazingira magumu zaidi.

Matamanio yake ni kuona elimu ikitolewa kwa usawa kama ilivyo sasa, lakini kundi la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu lingepatiwa fursa ya kusoma zaidi ili waje waokoe familia zao na kwa waliotoka katika mazingira magumu wanapaswa kuwakumbuka wenzao wanaoishi kama walivyokuwa wao siku za nyuma.

Jambo jingine, anasema angetamani Watanzania walifanye ni kutafakari namna ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kuzuia ufisadi, wizi na wawe na ndoto za kuwa na taifa bora lenye maono ya mbele.

Anasisitiza watu kufanya kazi na kujitafutia maarifa bila kuchoka.

Msomi huyo anasema serikali ya sasa inafanya mambo mengi makubwa na mazuri lakini watu wengi hawajaelewa mfumo mzima, ndiyo maana wanaishia kulaumu kuwa maisha ni magumu.

Balozi huyo alikwepa kuzungumzia masuala ya kisiasa na utendaji yakiwemo malalamiko ya wanasiasa kutoka upinzani, akisema mambo hayo kwake yatakuwa kinyume lakini anajua wote kwake ni Watanzania watakaomtegemea huko aendako.

Wasomi na siasa

Profesa Mbennah hakatai wala kukubali kuhusu umuhimu wa siasa, bali kwake anasema kila jambo analolifanya lazima kuwe na wito lakini bado hajawahi kupata ndoto wala wito wa kuwa mwanasiasa wa kugombea.

Alisema anawaheshimu wanasiasa na mchango wao katika taifa bali wanapaswa kutafakari kabla ya kugombea kujua ni nini wanataka kuwasaidia wapiga kura wao kwenye maeneo wanayotoka na kisha waone nini kinatakiwa kwa taifa.

Mbali na shughuli zake za ubalozi, Profesa Mbennah anatamani kuendelea kufundisha kama atakuwa na nguvu za kufanya hivyo na kuendelea kusaidia katika tafiti zitakazoleta matokeo chanya kwa nchi na watu wake.

Mbenah ambaye ni baba wa watoto wanne, anatamani Watanzania kuwa na umoja na mshikamano na kujali kufanya kazi na kujiendeleza katika kutafuta maarifa zaidi.