VIDEO: Mbowe: Hatutasusa uchaguzi, hatutokubali kuchakachuliwa matokeo

Muktasari:

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimesema kimesema kitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Kimewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura. Uandikishaji ulianza Oktoba 8 na utamalizika Oktoba 17, 2019.

Dar es Salaam. Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimesema hakitasusia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 20919 na hakitaruhusu kuchakachuliwa kwa matokeo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Oktoba 15, 2019 na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mbowe aamesema hawatoruhusu matokeo ya uchaguzi huo kuvurugwa na vyombo vya dola wala watumishi wa serikali.

Amesema japokuwa wamefungwa mikono kwa miaka minne kwa kutokufanya siasa watashiriki uchaguzi huo na wana uhakika watashinda.

“Wakijaribu kuvuruga au kuchakachua uchaguzi huu tutawatuma wananchi, serikali itambue kuwa wananchi wana ghadhabu,” amesema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni

“Watanzania waache uoga, hatuwezi kuingiza uoga, tukategemea tutabadilisha nchi haya ni mapambano ya kisiasa wacha watumie mbinu zao zote, sisi tutatumia nguvu ya umma kuhakikisha kuwa tunashinda,” amesema