Mbowe, Lipumba watoa kilio cha demokrasia kwa Rais Magufuli

Monday December 9 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mwenzake wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wametumia fursa ya kutoa salamu katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika kumwomba Rais John Magufuli kutumia nafasi yake kulea,  kulinda na kukuza demokrasia.

Sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika mjini Mwanza leo Jumatatu Desemba 9, 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba na kuhudhuria na watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na Serikali.

Profesa Lipumba ndiye aliyeanza kutoa ombi hilo baada ya Rais Magufuli kuwakaribisha viongozi wa vyama vya siasa waliokuwa wamekaa jukwaa kuu kusalimia wananchi.

Akitumia salaam ya chama chake cha “Haki” Profesa Lipumba amesema pamoja na hatua kubwa ya maendeleo inayopigwa, ni jukumu na wajibu wa Rais Magufuli na Serikali kuendeleza misingi ya demokrasia nchini.

Kauli kama hiyo pia ikatolewa na Mbowe akimueleza Rais Magufuli kuwa anayo dhamana ya kuhakikisha sio tu demokrasia inalindwa na kukuzwa, bali pia uwepo wa haki na usawa kwa wote bila kujali tofauti zao.

 “Nimeshiriki maadhimisho haya kuthibitisha misingi ya umoja, mshikamano na undugu miongoni mwa Watanzania. Nakuomba mheshimiwa Rais kutumia nafasi na dhamana yako kulinda demokrasia. Kusiwe na wanaofurahi huku wengine wakilalamika,” amesema Mbowe.

Advertisement

Viongozi wengine waliotoa salaam na kusisitiza mshikamano, umoja na ulinzi wa amani ya Taifa ni mwenyekiti wa UDP,  John Cheyo na mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, John Shibuda.

Viongozi wengine wastaafu waliokuwepo uwanjani hapo na kupata fursa ya kuzungumza ni marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Advertisement