Mbowe: Mashtaka yanayotukabili ni ya kisiasa, yanawaficha waliokosa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mashtaka yanayowakabili ni ya kisiasa, yanayoficha waliokosa na kuwahukumu waliokosewa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mashtaka yanayowakabili ni ya kisiasa, yanayoficha waliokosa na kuwahukumu waliokosewa.

Mbowe aliyeanza kujitetea Novemba 4 na 5, 2019 ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 mahakamani hapo akiongozwa na wakili,  Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Katika kesi hiyo Mbowe na wenzake wanane wanakabiliwa na   mashtaka 13 ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi  makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Mbowe ameeleza hayo baada ya kuulizwa na wakili Kibatala nini kauli yake kuhusu mashtaka yanayowakabili.

Wakili Kibatala wakati akiendelea kumuongoza Mbowe kutoa utetezi alimuuliza katika hati ya mashtaka liliibuka suala la kutompenda Rais John Magufuli, kumuuliza mbunge huyo wa Hai kama anampenda au anamchukia kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Katika majibu yake Mbowe amesema hamchukii Rais Magufuli ila anamshangaa, akibainisha kuwa ameshindwa kusimamia demokrasia katika Taifa.

Mbowe ameomba mahakama hiyo kupokea nyaraka mbalimbali kama kielelezo, zikiwemo barua kutoka Chadema kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kutoka tume hiyo kwenda Chadema pamoja na zile za kutoka ofisi ya msimamizi wa uchaguzi.

Mbali na Mbowe,  washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Wengine ni mbunge wa mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Halima Mdee (Kawe); Este Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini); John Heche (Tarime Vijijini); Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na  katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.