Mbowe aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa katika kituo cha Polisi Bomang'ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa zaidi ya saa mbili.

Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa katika kituo cha Polisi Bomang'ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa zaidi ya saa mbili.

Mbunge huyo wa Hai alikamatwa leo Ijumaa Februari 28, 2020 saa 12 jioni baada ya kumaliza kuhutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Nkoromu kata ya Masama Kati wilayani Hai.

Amehojiwa kuanzia saa 12:35 jioni hadi saa 3:20 usiku na alipotoka katika kituo hicho amewaeleza waandishi wa habari kuwa hawezi kuzungumza chochote.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamdun alilieleza Mwananchi kuwa Mbowe amekamatwa baada ya kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano huo.

Amebainisha kuwa maneno aliyoyatoa yanaashiria  uchochezi  na kuamsha hisia za wananchi, chuki dhidi ya Serikali ya Tanzania na polisi.

"Mbowe amekamatwa baada ya kutuhumiwa kusema au kutoa maneno yanayoashiria uchochezi, kuamsha hisia na chuki dhidi ya Serikali na polisi. Anahojiwa lakini baada ya mahojiano atapewa haki ya dhamana,” amesema kamanda Hamdun

Katika mkutano huo,  Mbowe amesema hawezi kupongeza utendaji kazi wa Serikali mpaka atakapokuwa na uhakika Serikali inatenda haki kwa watu wote.

Alikamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara saa 11:58 jioni

Wakati akijiandaa kuondoka eneo hilo, polisi walikwenda katika gari lake wakieleza kuwa wanamhitaji kituoni, ombi ambalo liliridhiwa na mwenyekiti huyo wa Chadema baada ya mvutano uliodumu takribani robo saa.

Awali, akizungumza katika mkutano huo Mbowe amesema licha ya kupitia  kipindi kigumu na changamoto mbalimbali za kisiasa, hawezi kukoma kuendelea na mapambano.

Huku akisisitiza kuwa hajawahi kupitia kipindi kigumu katika siasa kama sasa Mbowe amesema, “kufa sijafa lakini cha mtemakuni nimekiona, nimekaa jela, mahabusu na mahakamani nimekwenda lakini sikomi ng'o, ndio kwanza wananitia moto.”

Amesema haogopi kufa wala kwenda jela, huku akigusia umuhimu wa kujenga miundombinu ya barabara na reli na kuwaacha wananchi kuwa huru.

"Hakuna kitu chenye thamani katika maisha yenu kama uhuru wenu, mkijengewa barabara, shule lakini mkanyimwa uhuru wenu ni bora mvikose hivyo vyote lakini mpate uhuru wenu na hayo ndiyo maneno ambayo Chadema tumehubiri,” amesema Mbowe.

Mbunge huyo wa Hai amesema wananchi wanahitaji nchi ya demokrasia, wote walindwe, “mkiwa Chadema mlindwe, CCM nao walindwe, kila mmoja katika nchi hii ajione kuwa ni raia mwenye haki na awe na uhuru.”

Amesema wanahitaji askari walinde mikutano kwa amani na wananchi waone raha ya kwenda kwenye mikutano, na si kuwajaza hofu.

Aliwaondoa hofu wananchi kutokana na kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba hata kama atafungwa, akitoka mapambano yataendelea.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amewaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa amemuandikia barua Rais John Magufuli  kutaka uchaguzi wa Serikali za mitaa urudiwe nchi nzima.

“nimemuandikia Rais barua nimemwambia Chadema kama chama kikuu cha upinzani hawawatambui wenyeviti wa Serikali za mitaa waliochaguliwa, tunahitaji  uchaguzi urudiwe nchi nzima ili wapatikane viongozi waliochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi,” amesema Mbowe.

Mbowe leo ndio ameanza ziara ya siku tano katika jimbo la Hai inayoambatana na mikutano ya hadhara, na amebainisha kuwa kesho Februari 29, 2020 atazungumza mapema na wananchi wa eneo la Bomang'ombe.