Mbowe adai polisi walihusika mauaji mwanafunzi NIT

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema huenda aliyempiga risasi aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na kufariki dunia ni polisi.

Dar es Saalam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema huenda aliyempiga risasi aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na kufariki dunia ni polisi.

Mbowe ameeleza hayo leo Jumanne Novemba 5, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akijitetea katika kesi inayomkabili.

Amesema Jeshi la Polisi linaweza kuwa linahusika kutokana na kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai amesema katika mkutano na waandishi wa habari, Mambosasa alisema jeshi hilo linawashikilia askari wake kwa uchunguzi.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na mashtaka 13 katika kesi ya jinai namba 112/2018.

Akiongozwa na wakili Peter Kibatala, mwenyekiti huyo wa Chadema amesema alipata taarifa kuhusu kifo cha Akwilina aliyepigwa risasi katika maandamano ya chama hicho kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

"Kwa ufahamu wangu na hadi leo natoa ushahidi wangu mahakamani ninaweza kusema aliyempiga risasi Akwilina  ni askari polisi.

“Hiyo ni kutokana na taarifa aliyoitoa kamanda Mambosasa alipofanya mkutano na waandishi wa habari. Alisema jeshi lake linawashikilia baadhi ya askari polisi kwa ajili ya uchunguzi,” amesema Mbowe.

Alipoulizwa kuhusu ushiriki wake katika maandamano yanayodaiwa kufanywa na viongozi wa chama hicho  kutoka viwanja vya Buibui hadi ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mbowe amedai hakuwepo kwenye maandamano hayo na alitajwa kwa hisia.

Amebainisha kuwa baada ya kumaliza mkutano wa kufunga kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni katika viwanja vya Buibui aliondoka akiongozwa na  askari polisi kuelekea ofisi za makao makuu ya chama hicho, Kinondoni.

Amesema baada ya mkutano kumalizika waliohudhuria wakiwa njiani walikutana na wanachama wa CCM waliokuwa wametoka katika mkutano eneo la Morocco na Mwananyamala.

“Walikuwa na mgombea wao katika gari la wazi huku akisindikizwa na kikundi cha ngoma maarufu kama mdundiko,” amesema Mbowe.

Amesema wanachama wa Chadema walikuwa wakiongozwa na polisi kuelekea barabara ya Morocco na hakuwa akijua kinachoendelea kwa maelezo kuwa alikuwa akielekea makao makuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Amesema kati ya washtakiwa walio katika kesi hiyo hakuna aliyekamatwa eneo la Mkwajuni.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza utetezi wa mshtakiwa huyo ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, 2019 siku ambayo Mbowe ataendelea kujitetea.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine ni manaibu katibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda); Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); Esther Matiko (Tarime Mjini) na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13 ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.