VIDEO: Mbowe aeleza mkakati wa Chadema kutotegemea ruzuku

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza mkakati mpya ya kidigitali utakaokiwezesha chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kutotegemea ruzuku ya Serikali.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza mkakati mpya ya kidigitali utakaokiwezesha chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kutotegemea ruzuku ya Serikali.

Amesema mkakati huo ni kukusanya ada ya wanachama itakayofikia Sh15 bilioni kwa mwaka, akibainisha kuwa inatosha kukiendesha chama hicho.

Kwa mujibu wa Mbowe, kwa sasa Chadema kinapata ruzuku ya Sh280 milioni kwa mwezi.

Mbowe amesema programu hiyo iliyozinduliwa leo Jumatano Desemba 18, 2019 inahusisha uandikishaji wa wanachama kidigitali, kufanya mikutano kidijitali pamoja na kampeni.

Ametoa kauli hiyo leo katika mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika katika ukumbi wa  Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Kila mwaka mwanachama anatakiwa alipie Sh1,000 ya ada, kwenye vikao hivi tunapendekeza iwe Sh2,500 kwa mwaka. Maana yake ni nini? Leo hii chama kinapata ruzuku ya Sh3 bilioni kwa mwaka. Gharama ya kufanya mkutano wa baraza kuu ni zaidi ya Sh1 bilioni kwa hiyo ruzuku peke yake haitoshi.”

“Kupitia Chadema Digital tuna digital fund raising (Harambee ya kidigitali), tumekubaliana kuchangia Sh2,500. Asilimia 90 wana Chadema wana simu za mkononi, kila mwanachama akilipa kwa simu tutapata Sh15 bilioni kwa mwaka.”

Amesema kupitia vikao vyao wataibadilisha katiba ya Chadema ili kuruhusu mfumo huo ufanye kazi vizuri, “tunahitaji kujenga chama cha kujitegemea na hili msajili usikie, maana yake kuna watu wanafikiri chama kinategemea sana ruzuku.”

Amesema kutokaa na mfumo huo, chama hicho sasa hakihitaji tena kufanya mikutano ya hadhara ili kupata wanachama wapya.

“Tumesema mikutano ya hadhara hatuitaki tena, tutaifanya wakati wa uchaguzi. Tumefanya kampeni kimyakimya, tumefanya nyumbani kwa watu, kwa wavuvi, mabondeni. Tumegundua Chadema ipo mioyoni mwa watu.”

“Kama chama kimeandikisha wanachama 50,000 wakalipa Sh2,500 maana yake jimbo moja Sh125 milioni. Kuanzia Januari ni wajibu wa viongozi, kuhakikisha kila mwanachama anasajiliwa kwenye Tehama. Kwa kadiri wanavyochangia zaidi ya nusu ya pato litarudi jimboni.”

Amesema kila jimbo litarudishiwa zaidi ya nusu ya fedha hizo kwa ajili ya kujenga ofisi, kununua magari, kulipa mishahara ya watumishi na kununua vitendea kazi.

“Katika mabadiliko ya katiba tunayofanya tunaingiza digital fundraising ambayo ni Sh2,500 kwa kuwa mwanachama wa Chadema. Unaweza kuridhia hiyo hela ikatwe bila hata wewe kutuma. Kwa hiyo kuanzia mwaka ujao, ruzuku ni kama supplementary, wakitaka kwenda nayo waende,” amesema Mbowe.