Mbowe aizungumzia kauli ya Jaguar, aitaka Kenya kuchukua hatua

Muktasari:

Siku moja baada ya kauli ya mbunge huko Kenya, Charles Kanyi maarufu ‘Jaguar’ kuhamasisha wananchi wake kuwaondoa wafanyabiashara wageni nchini humo, Kiongozi wa Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe ameitaka Serikali ya Kenya kujitokeza na kupinga kauli hiyo.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe ameitaka Serikali ya Kenya kukanusha kauli iliyotolewa na mbunge wa jimbo la Starehe nchini humo, Charles Kanyi maarufu Jaguar na kuhakikisha kauli kama hizo hazijirudii tena.

Jana Jumanne, video fupi ya Jaguar ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha mbunge huyo akihamasisha wananchi kuwaondoa raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania ambao wanafanya biashara kwenye masoko yaliyopo jimboni kwake.

Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumatano Juni 26, 2019, Mbowe amesema kauli hiyo inayojenga chuki dhidi ya wageni (xenophobia) imesababisha usumbufu siyo kwa Tanzania pekee bali katika ukanda mzima wa Afrika.

 

 “Wakenya wanatakiwa kujitokeza na kuikataa kauli hiyo. Inachafua hadhi na nafasi ya Kenya ambayo imejengwa kwa miaka mingi,” amesema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema

Amebainisha kwamba Kenya ndiyo itaathirika zaidi kwa sababu nchi za Afrika ndiyo zinatengeneza soko kubwa la bidhaa na huduma kutoka Kenya kuliko nchi nyingine yoyote isipokuwa Afrika Kusini.

 

Mbowe amesema Kenya imekuwa ni kitovu cha nchi mbalimbali za Afrika kwa miaka mingi, jambo ambalo limeufanya mji wa Nairobi kuwa wa kibiashara na uwekezaji katika ukanda huu wa Afrika.

 

“Binafsi nina imani na uongozi wa Kenya. Unatakiwa kuchukua hatua na kukomesha upuuzi huo ili kurudisha umoja, undugu na upendo katika ukanda huu,” amesema Mbowe na kuongeza kuwa kauli hiyo imesababisha taharuki za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia.

Jana jioni bungeni, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu suala hilo alisema Serikali ya Kenya imemkana Jaguar.

“Serikali ya Kenya wametutaka tuwe watulivu na kumtaka Jaguar kusema kauli hiyo ameipata wapi na alikuwa akimaanisha nini. Sisi Watanzania  maeneo yote tulipo kama tuna ndugu zetu Wakenya tuishi nao vizuri na hatuna chuki nao na wao hawana chuki na sisi,” alisema Majaliwa