VIDEO: Mbowe akemea kauli za ubaguzi

Muktasari:

Ibada ya kumuombea Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 2019 imefanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Moshi Mjini

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amekemea kauli za ubaguzi wa dini, rangi, ukabila na kisiasa wakati akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kumuombea aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi inayofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Moshi Mjini.

Mbowe akizungumza leo, Alhamisi, Mei 9, 2019 kabla ya kuanza kwa ibada hiyo, amezungumzia amesema

heshima pekee ambayo Watanzania wanaweza kumpa Mengi atakayezikwa leo kijijini kwao, Nkuu, Machame ni kutafakari na kuyaishi yale mema aliyokuwa akiyafanya hasa kuwa mnyenyekevu, kauli zake zilizojenga, kupatanisha na kutoa matumaini.

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, amesema ni vyema kuchunga kauli zinazotolewa kama zikaweza kujenga, lakini siyo kuwagawa watu katika makundi.

“Kipekee kabisa mnisamehe, niseme jambo moja ambalo limetukwaza wengi na kwa sababu sina tabia ya unafiki nitasema ‘straight’ ni nchi moja ambayo tunastahili kupendana, kujengana, kuheshimiana na kumuona kila mmoja wetu ni sehemu ya nchi,” amesema.

“Tusikubali matendo na kauli za kibaguzi zikatubagua katika nchi yetu, tutapoteza Utanzania wetu sifa ambayo tumejivunia kwa miaka mingi.”

Kauli hii ya Mbowe iliwafanya waombolezaji wa ndani na nje kushangilia kwa kupiga makofi.

“Anapotokea kiongozi mwenye mamlaka akatoa kauli ya kubeza kabila fulani, tukaanza kubaguana kwa makabila au kwa dini siyo mambo mema, lazima wote tuungane kila mmoja kwa nafasi yake tukakemea jambo hili,” amesema Mbowe.

“Tusianze kubaguana kwa itikadi, tusibaguane kwa imani, tusibaguane kwa makabila yetu, tupendane na  kutambuana kama Watanzania, kauli za kuambiana kuwa kuna kabila fulani haliwezi kuwatetea walemavu si za kweli ni za kibaguzi na lazima tuzikemee.”

Mbunge huyo wa Hai pia akasema, “naomba wote walioguswa na kauli zile tutoe msamaha kumuenzi mzee wetu Mengi, tusamehe, lakini tusiwe wanafiki tujifunze kusema ukweli na kweli itawaweka huru.”

Amesema katika mazingira ya kibinadamu kuna mambo mawili yanayojenga kiburi ambayo ni mamlaka yasiyotumiwa vizuri na fedha zisizotumika kwa unyenyekevu.

“Mzee Mengi hakuwa kiongozi wa kisiasa, lakini alikuwa mnyenyekevu, utajiri wake haukumtia kiburi, bali ulimuongezea unyenyekevu na msaada kwa wengi ambao aliwajua na ambao hakuwajua.”

Mbowe amesema, “hivyo kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani. Niombe sana Watanzania wenzangu kama tulivyokuwa kwa pamoja na kukaa pamoja kwa dini zote, kabila zote, vyama vyote niombe basi tuuendeleze unyenyekevu kwa siku zote na siyo tuuonyeshe tunapokuwa kwenye matatizo.”

Viongozi mbalimbali wamejitokeza kanisani hapo akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Said Mwema; mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya mbalimbali nchini.