Mbowe alivyopishana na Mashinji mahakamani

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepishana na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji baada ya wote kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na wenzao saba.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepishana na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji baada ya wote kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na wenzao saba.

Kutokana na kufika mahakamani muda tofauti wawili hao hawakuweza kusalimiana.

Awali, Dk Mashinji alisalimiana na wenzake ila mbunge wa Kawe, Halima Mdee alikataa kumpa mkono katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema.

Februari 18, 2020 Dk Mashinji alihamia CCM  huku akikosoa uongozi na uendeshaji wa Chadema.

Mahakama hiyo imepanga Machi 20, 2020 kutoa hukumu ya kesi inayowakabili viongozi nane wa Chadema pamoja na Dk Mashinji.

Katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kati ya Februari 1 na 16, 2018.

Uamuzi wa mahakama umetolewa leo Jumatatu Februari 24, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Mbali na Mbowe, Dk Mashinji na Mdee, washtakiwa wengine ni katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Ilivyokuwa

Leo mahakamani  walianza kuingia washtakiwa wengine huku Mbowe akiwa wa mwisho kuingia na kwenda

kuketi na mbunge wa Kawe, Halima Mdee. Dk Mashinji alikuwa amekaa na ofisa habari wa chama hicho,  Tumaini Makene.

Baada ya kesi kuanza walipanda kizimbani wakati huo Dk Mashinji akikuwa ameketi  kiti cha nyuma na Mbowe alikuwa amekaa mbele.

Kesi hiyo ilipoahirishwa Mbowe alianza kutoka na Dk Mashinji alikuwa wa mwisho kutoka.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema alipotoka alianza kusalimiana na watu mbalimbali, wakati huo Mbowe alikuwa ameshaondoka.