Mbowe amshukia Ole Sabaya mwenyewe amjibu

Muktasari:

Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe amesema kama Rais John Magufuli hata  mwondoa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ole Sabaya akidai kuwa anawabambikizia watu wema kesi na kuidhalilisha wilaya ya Hai atapambana naye.

Hai. Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe amewashukia mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo (OCD), akiwatuhumu kuwabambikia raia wema kesi.

Kauli hiyo imekuja miezi michache baada ya Sabaya kuwatuhumu wafanyabiashara wawili mashuhuri kwa kuhujumu miundombinu ya reli lakini polisi mkoani Kilimanjaro wakawasafisha na tuhuma hizo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja ya Snow View, Mbowe ameenda mbali na kumtaka Sabaya na OCD kuacha kuwabughudhi madereva wa bodaboda wanaomuunga mkono.

“DC Sabaya anabambikizia watu kesi  zisizokuwa na msingi, anawatuhumu watu kuharibu miundo mbinu ya reli kitu ambacho sio cha kweli, vijana wa bodaboda Hai hawaishi kwa amani eti kisa wanamuunga mkono Mbowe anawaambia eti mtakiona,”

“Eti mnaenda kwenye vituo vya bodaboda kuwazuia wasimpokee mbunge wao mambo gani ya kihuni haya? isitoshe kila mtu anayekuja kwenye mkutano wa Mbowe anasumbuliwa, DC nakwambia utamjua Mbowe ni nani.”

“DC Sabaya usione tunakuogopa, tulikaa mbali tunakucheka tuu, lakini ninamwambie Rais Magufuli ametuletea DC muhuni na kama hutamwondoa sisi watu wa Hai tutapambana naye kihuni,” anasema Mbowe.

Mbunge huyo amedai kuwa wapo vijana wanaojiita ni Sabaya wanatokea Arusha, wamekwenda Hai kunyanyasa wananchi na kuwatesa.

“Tulikaa mbali  tukaona utazoea, sasa hutaki kuzoea tutapamba na wewe kwenye majukwaa, sijawahi kuona DC wa sampuli hii. Anaongoza genge la wahuni na siogopi kusema, hao vijana wake wanaojidai ni usalama wa Taifa tunawajua, tunakupa muda jirekebishe , hapa Hai utaondoka kama walivyoondoka Ma- DC wengine,” amesema Mbowe

Amemtaka Ole Sabaya kama anataka kufanya kazi yake vizuri Hai, ni vema akajishusha kwa kuwaheshimu wananchi anaowaongoza na watumishi wenzake wa Serikali.

“Usione madaraka ya kupewa ukaona ni bora kuliko wengine, umechafua na kuidhalilisha wilaya ya Hai na watu wanaogopa kusema, mimi sikuogopi, tunataka Taifa la watu wenye amani na uhuru,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Mkuu huyo wa Wilaya kusudi azungumzie tuhuma hizo, alisema hawezi kumjibu Mbowe.