Mbowe amuandikia barua Magufuli, amuomba mambo matatu

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemwandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli akiomba mambo matatu likiwemo la marekebisho ya katiba yatakayozaa tume huru ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemwandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli akiomba mambo matatu likiwemo la marekebisho ya katiba yatakayozaa tume huru ya uchaguzi.

Katika barua hiyo iliyotumwa Ikulu Januari 29, 2020,  Mbowe ametaka uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019 kufutwa na kuanza mchakato wa maridhiano ya kitaifa.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai ameeleza hayo leo Jumatatu Februari 3, 2020 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari.

Amesema mambo hayo matatu yasiposhughulikiwa Chadema isilaumiwe kwa yatakayotokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.

"Huu ni mwaka wa uchaguzi, kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa kama hatutazika viburi vyetu vya kiitikadi na kusimama pamoja," alisema Mbowe.

Mbowe amekumbusha wito wake wa kutaka maridhiano alioutoa Desemba 9, 2019 jijini Mwanza katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia aligusia kauli ya Magufuli kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa huru na haki.

"Ukimya wetu sio woga. Tuna wanachama wengi tunaofanya kazi ya ziada kuwatuliza. Subira ina mwisho siku yakifika ya kufika tusilaumiwe," amesema Mbowe.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, Mbowe ametaka ufutwe na urudiwe.

"Kufutwa kwa uchaguzi huu kutahalalisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu (uchaguzi mkuu) utakuwa huru na wa haki. Uchaguzi huu ukafanyike sambamba na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais.”

"Kama CCM ikitupeleka kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa ule wa serikali za mitaa, hii nchi haitakuwa salama,” amesema Mbowe.

Kuhusu maridhiano, amesema wamemwandikia Rais Magufuli barua afikirie kuunda tume ya maridhiano ili kusikiliza malalamiko ya wananchi.

Ametaja baadhi ya mambo yanayotokea nchini na kuhitaji maridhiano ni pamoja na watu kupotea, miili ya watu kuokotwa katika fukwe za bahari, kesi za kisiasa na wakosoaji wa serikali na kuwepo katazo la kufanya siasa.