Mbowe amwombea ruhusa Sugu kwa mkewe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Muktasari:

  • Leo Jumamosi Agosti 31, 2019 mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ amefunga ndoa na Happiness Msonga katika Kanisa Katoliki Ruanda jijini Mbeya.

Mbeya. Leo Jumamosi Agosti 31, 2019 mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ amefunga ndoa na Happiness Msonga katika Kanisa Katoliki Ruanda jijini Mbeya.

Baada ya misa hiyo, wanandoa hao waliungana na ndugu na jamaa nyumbani kwa wazazi wa mbunge huyo ambako wageni mbalimbali walifika kumpongeza akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni alikuwa kivutio alipowasili na  kati ya mengi aliyozungumza ni kumwombea ruhusa Sugu kwa mkewe.

“Hongera sana Sugu na mkeo Happiness lakini niseme mama yetu (Happness) Sugu ni kiongozi hivyo usimzuie pale tutakapomhitaji kutekeleza majukumu ya kitaifa,” amesema Mbowe.

Sugu alilieleza Mwananchi kuwa ameamua kufanya sherehe eneo hilo kwa kuwa kufunga ndoa ni baraka si starehe au burudani na kutaka kila anayejisikia kufika kwa ajili ya kumpongeza afanye hivyo.

Baadhi ya wabunge waliohudhuria sherehe hiyo ni wakiongozwa na Meya wa Jiji la Mbeya,  David Mwashilindi ni  Frank Mwakajoka (Tunduma);  Anthony Komu (Moshi Vijijini); Lucia Mlowe, Sophia Mwakagenda na Lucy Mollel (wote Viti Maalum).

Wengine ni Joseph Haule (Mikumi); Joseph Selasini (Rombo); David Silinde (Momba); Pascal Haonga (Mbozi) na Wilfred Lwakatare (Bukoba  Mjini).