Mbowe ashauri kuundwa kikosi kazi cha corona

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Hotuba ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe ameshauri kuundwa kwa kikosi kazi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za kiuchumi zinazotoakana corona.

Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Bunge nchini Tanzania, Freeman Mbowe ameshauri kuundwa kwa kikosi kazi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi zitakazotokana na ugonjwa wa corona.


Mbowe amesema hayo leo Jumatatu Aprili 6, 2020,wakati akichangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/2021.


Amesema kuwa suala la corona halijapewa uzito unaostahili na kwamba ni wajibu kushirikiana wote kwa kulipa uzito unaostahili.


Amesema bado suala hilo halijapewa uzito unaostahili kama mataifa mengine kwasababu bado kuna uzembe kwa kujua ama kutojua au kudhani liko mbali  na halipo nchini.

Amesema alitegemea uwepo wa mpango maalum na kutoa taarifa iwapo kuna athari gani katika uchumi lakini bajeti ziko pale pale.
Amesema kuwa sekta ya utalii imeanguka kwa asilimia 99 na kwamba kuna makampuni yamefungwa.
Amesema kuwa mapato ya nchi yatapungua kwa asilimia 40 kwa miezi sita ijayo


Mbowe amesema kumekuwa na kauli tofauti, mikusanyiko ambayo haifai na kwamba kuna mikusanyiko ambao wakuu wa mikoa ndio wamekuwa wakiifanya.


“Wanakusanya watu, wanahutubia watu kwamba ugonjwa uko mbali hii ni hatari. Sasa Serikali inasema nini? Tumsikile nani. Ningetamani tumesikilize Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Afya,”amesema.


Amesema kama nchi ikienda kwa kila kiongozi kutoa taarifa ugonjwa huo utawafikisha mahali pabaya na kushauri ni bora Serikali kujiandaa hata kama ugonjwa uko mbali.


Ametaka kujifunza katika nchi nyingine kwa kuangalia nchi nyingine zinafanya nini katika kupambana na ugonjwa huo.
Amesema jambo hilo linahitaji kikosi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi na kijamii na pia kuangalia vipaumbele vya Taifa hivi sasa ni kipi.


“Lazima tususpend baadhi ya mipango ili kuwezesha kukabiliana na tatizo hili,”amesema.
Kuhusu uchaguzi ametaka kutengenezwa kwa maridhiano ya Kitaifa kwa kutengeneza Tume huru ya uchaguzi na kwamba uchaguzi ni process ambayo inajumuisha uandikishaji, upatikanaji wa vifaa na urekebishaji wa sheria.


Amesema wamekuwa wakidai mabadiliko ya sheria kwa sababu wanaamini ili nchi iweze kuendelea vizuri inahitaji kupata viongozi wanaopatikana kwa njia ya kidemokrasia.


Amesema jambo hilo linahitaji utashi wa kisiasa sio kwa kushindana kwa kupiga kelele


“Mimi nimemwandikia mheshimiwa Rais, mara nyingi tumezungumza katika forum mbalimbali jamani tunahitaji marekebisho machache ya sheria,”amesema.


Amesema  wakati mchakato wa Katiba mpya unashindikana walikubaliana na Rais Jakaya Kikwete waende katika marekebisho machache ya sheria hadi hapo Katiba itakapokamilika.
Amesema kuwa kifungu namba 74 na 75 ya Katiba inahitaji marekebisho machache na kwamba kama kuna
utashi wa kisiasa mambo hayo yanawezekana.


Amesema ili watu waende katika uchaguzi wamekubaliana na kuridhiana na hivyo kupata viongozi waliopatikana kwa demokrasia na si kwa ghiliba.


Amesema kuna wagombea wanaoenguliwa kwa sababu ya makosa madogo madogo kama kukosa kuweka nukta.


Amesema kuwa muda wa kufanya hivyo upo kama kuna utashi wa kisiasa kwa sababu haihitaji fedha kufanya maboresho madogo ya sheria za uchaguzi na Katiba katika vifungu hivyo viwili.