Mbowe ataka wadau kukutana kabla ya uchaguzi mkuu 2020

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali ya Tanzania kukaa na wadau kutafuta njia bora ya kwenda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 kutokana na vyama vya siasa kubanwa kufanya mikutano ya hadhara tangu mwaka 2016.

 

Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali ya Tanzania kukaa na wadau kutafuta njia bora ya kwenda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 kutokana na vyama vya siasa kubanwa kufanya mikutano ya hadhara tangu mwaka 2016.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 6, 2020 katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni mjini Dodoma.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai alianza kwa kuhoji sababu za vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya kazi za uenezi.

“Unajua vizuri sana Serikali yako inajua vizuri sana, Watanzania wanajua vizuri sana kwamba vyama vya siasa vya upinzani vimezuiwa miaka minne sasa kufanya kazi na uenezi,” amesema Mbowe.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amehoji ni sheria ipi iliyotumika kuzuia mikutano hiyo, akijibu alichokieleza awali Majaliwa kuwa kuzuiwa kwa mikutano hiyo ni utaratibu uliowekwa.

“Mmejiwekea kwa sheria ipi? Unajua yote hayo unajua vizuri sana, kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeandikwa katika Katiba kuwa huru lakini sio huru,” amesema Mbowe.

Amesema majibu ya Majaliwa kuhusu suala hilo ni mepesi na kuna siku watakuja kujuta kwa majibu hayo mepesi.

“Waziri Mkuu hamuoni ni wakati muafaka sasa Serikali kukaa na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya uchaguzi kutafuta njia bora ya kwenda katika uchaguzi wa Oktoba kuliko kwenda kibabe kama mnavyotaka kwenda,” amehoji.

Katika majibu yake Majaliwa amesema Serikali haiongozi kibabe.

“Mheshimiwa Mbowe tunazungumza tunabadilishana mawazo, tunapobadilishana mawazo tunalenga katika kulifanya Taifa hili liwe na usalama liwe na utulivu ili shughuli zetu ziweze kwenda tu, lakini pia Watanzania wanahitaji maendeleo,” amesema.

Majaliwa amesema wanapokea utaratibu wa namna ya kufikia wananchi na kupata maendeleo sio suala la chama kimoja bali ni la Watanzania wote.

“Hakuna diwani wala mbunge aliyezuiliwa kufanya mkutano katika eneo lake. Inaweza kuwa kama kuna tatizo mahali fulani, kwa utaratibu huo tunazungumza, tunakutana, tuambizane wapi kuna shida,” amesema Majaliwa.

Amesema kuwa wiki iliyopita Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi alisema kuwa kuna zuio la mkuu wa polisi wa wilaya.

 “Na mimi nilimwita hapa mkuu wa Mkoa  anaungana naye, mkuu wa polisi mkoa ameungana naye. Shida kama iko kwenye eneo dogo huko tunazungumza.”

“Nataka nikuhakikishie kiongozi wa kambi ya upinzani nakuheshimu sana, tunatambua majukumu kwa  chama chako lakini pia Serikali inaendelea kushirikiana na viongozi wa vyama vyote ili Taifa hili liendelee kuwa salama na utulivu,” amesema Majaliwa.

Kuhusu tume huru ya uchaguzi, Majaliwa amesema katiba na utendaji wa tume hiyo uko huru na kwamba panapoonekana kuwa na tatizo ielezwe.

Majaliwa amesema hawajawahi kuona Rais, vyama vya siasa kuingilia  shughuli za chombo hicho na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ipi huru kama inavyoelezwa katika katiba.