VIDEO: Mbowe awataka Watanzania wajitokeze kujiandikisha

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

Kiongozi wa Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amewataka Watanzania kuweka kando tofauti zao na kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019.

Amesema kususia uchaguzi huo hakuwezi kuwa na tija kwani itawaondolea nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Mbowe amesema hayo leo Jumanne Oktoba 15, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema Kinondoni jijini Dar es Salaam kuhusu shughuli hiyo ya uandikishaji iliyoanza Oktoba 8 hadi 17, 2019.

Amesema uchaguzi huo ndio unawaleta viongozi wanaokwenda kutatua changamoto za wananchi hivyo kuacha serikali ifanye uamuzi ni kosa.

“Tunapaswa kuweka kando tofauti zetu, twendeni kwa wingi tukajiandikishe ili tushiriki kwenye uchaguzi huu muhimu,” amesema Mbowe

Amesema kinachotokea sasa ni matokeo ya serikali iliyopo madarakani kuweka msisitizo katika kukandamiza upinzani na kuwazuia watu wa upinzani kuchaguliwa.

“Kwa miaka minne, tunazuiwa kufanya siasa halafu leo una lazimisha watu kujiandikisha wamchague nani na ndiyo maana tunaona watu wanasusia yanayoendelea yanawafanya waandamane mioyoni mwao.”

“Leo tumeona tutumie siku tatu zilizobaki kuhamasisha watu waende kujiandikisha na washiriki kwenye uchaguzi na wala wasisusie,” amesema Mbowe

“Ni makosa makubwa na aibu kususia. Kwa muda wa siku tatu zilizoongozwa, viongozi wote wa kada zote, wahamasishane watoke kwa wingi kwenda kujiandikisha, hatuna sababu za kususia kwani tutakuwa tumesusia maisha yetu,” amesisitiza Mbowe

“Tunakwenda kushiriki uchaguzi huu na tutashinda, hatutakuwa woga na haya ni mapambano ya kisiasa, tutatumia nguvu za umma kuhakikisha tunashinda uchaguzi huu.”