Mbowe atua Kigoma, azindua tawi la Chadema jimboni kwa Zitto

Muktasari:

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe jana Jumamosi amezindua tawi maarufu la chama hicho la Urusi lililopo Mwanga katika Jimbo la Kigoma Mjini linaloongozwa na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo)

Kigoma. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amesema kibano wanachokipata wapinzani kutoka Serikalini kinatokana na hofu waliyonayo viongozi wa chama tawala cha CCM.

Amesema hofu hiyo inatokana na CCM kuhofia kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020 kwa Chadema kuibuka mshindi na kuongoza dola.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alitoa kauli hiyo jana Jumamosi Mei 4 wakati anazindua tawi maarufu la Chadema la Urusi lililopo Mwanga mjini Kigoma.

Tawi hilo lipo katika jimbo la Kigoma Mjini linaloongozwa na Zitto Kabwe wa ACT- Wazalendo.

Alisema viongozi na wanachama wa CCM wana hofu ya kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao, hivyo kuamua kuzuia mikutano ya hadhara na kuhakikisha viongozi wa vyama vya upinzani wanafunguliwa kesi mahakamani kila uchao.

"CCM wapo hoi, wamelegea ndio maana vyama vya upinzani vinapata kibano kwa viongozi wake kukamatwa, kupigwa na hata kuumizwa," alisema Mbowe.

Licha ya kukiri kutambua mchango wa wakazi wa mkoa wa Kigoma katika kujenga siasa za mageuzi tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Mbowe aliwataka wanachama kujenga upendo na umoja.

"Tumieni tawi hili la Urusi kufanya siasa za kistaarabu mkidumisha umoja na upendo miongoni mwenu na jamii nzima kwani huo ndio msingi wa chama chetu (Chadema)," alisema Mbowe.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kigoma, Ally Kisala alisema tawi la Urusi ni ngome muhimu ya Chadema mkoani Kigoma kwa kuwa linatumika kuelimisha jamii bila kubagua itikadi zao za kisiasa.

Katibu wa tawi la Urusi, Hamis Mkamba alisema baada ya viongozi wa awali kulegea na kuuza bango la tawi hilo kwa chama kimojawapo cha siasa kwa Sh14 milioni walilazimika kuhamia eneo jirani na kufungua tawi jipya.

"Urusi mpya ilianza mwaka 2014 ambapo tulijenga bango tunaloandika mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya mkoa wetu (Kigoma) ikiwa ni kero na changamoto zinazogusa maisha ya watu," amesema Mkamba.

Mkazi wa Mwanga mjini Kigoma, Aisha Shaban aliesema uzinduzi huo utaongeza hamasa kwa wanachama na kujenga upya Chadema iliyoyumba tangu mwaka 2015 mjini humo.

Eneo lilipo tawi la Urusi limejizolea umaarufu hususan wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa ambapo jeshi la polisi huimarisha ulinzi ili kuepusha rabsha.