Mbowe kufanya mikutano ya hadhara siku tano mfululizo

Muktasari:

  • Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe kuanzia leo Ijumaa Februari 28, 2020 atafanya mkutano wa hadhara katika jimbo hilo kwa siku tano mfululizo.

Hai. Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe kuanzia leo Ijumaa Februari 28, 2020 atafanya mkutano wa hadhara katika jimbo hilo kwa siku tano mfululizo.

Akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Februari 27, 2020 katibu wa Chadema Wilaya ya Hai, John Munis amesema polisi wamewapa kibali cha kufanya mikutano hiyo.

“Mbowe atakuwa na mkutano wa hadhara, atazungumza na wananchi wake pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili.”

“Mikutano hiyo itafanya kwa siku tano mfululizo, kuanzia kesho Ijumaa  hadi Jumanne ijayo katika sehemu mbalimbali za Wilaya ya Hai,” amesema Munis.

Amesema kesho Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni atafanya mkutano katika viwanja vya Nkoromu kata ya Masama kati.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni amesema polisi wana taarifa ya mkutano huo.

'”Kiutaratibu mbunge  anapokuwa na mikutano yake  anapaswa kutoa taarifa kituo cha polisi wilaya na taarifa za mkutano wa Mbowe tunazo,” amesema Kamanda Hamduni.