Mbunge CCM ahoji mikakati Serikali ya Tanzania kuboresha elimu

Mbunge wa Viti Maalum (CCM),  Zainab Katimba.

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali  kuhakikisha mfumo wa elimu unakidhi mahitaji ya soko kitaifa, kikanda na kimataifa kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali  kuhakikisha mfumo wa elimu unakidhi mahitaji ya soko kitaifa, kikanda na kimataifa kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema hayo leo Ijumaa Aprili 3, 2020 alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM),  Zainab Katimba.

Katika swali lake Zainab alitaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mfumo wa elimu nchini.

Akijibu swali hilo, Profesa Ndalichako amesema uboreshaji wa utoaji wa elimu katika nchi yoyote ni suala endelevu ambalo hutegemea mabadiliko yanayotokea katika nchi kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii  pamoja na ulinganisho wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.

 

Amesema nchini  suala la uboreshaji wa mifumo ya elimu limekuwa likifanyika na hutegemea tathmini mbalimbali za kitaalamu zinazofanyika kwa nyakati tofauti.

Akatoa mfano elimu ya sekondari ya chini (O-Level) kutambuliwa kuwa ni sehemu ya elimu msingi kwa watoto na inatolewa bila malipo ya ada.

Aidha, amesema katika elimu ya ualimu wameongeza miaka ya kumwandaa mwalimu wa elimu ya awali kutoka miaka miwili hadi miaka mitatu.

Ndalichako amesema pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeendelea na uimarishaji wa elimu kuwa ya umahiri kutoka katika mfumo wa awali ambao ulimwandaa mhitimu kwa nadharia bila mafunzo kwa vitendo ya kutosha.

Amesema uboreshaji huo umefanyika sambamba na uimarishaji wa mitaala katika ngazi zote.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mfumo wa elimu unakidhi mahitaji ya soko kitaifa, kikanda na kimataifa kwa ustawi na maendeleo ya nchi.