Mbunge CCM ahoji ukakasi uliopo kutekeleza PPP Tanzania

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) nchini Tanzania, Peter Serukamba 

Muktasari:

Mbunge wa Kigoma Kaskazini nchini Tanzania (CCM) Peter Serukamba amezungumzia kuhusu umuhimu wa Serikali kuingia ubia na Sekta Binafsi (PPP) ili kuchochea zaidi maendeleo.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) nchini Tanzania, Peter Serukamba amesema haelewi kuna ukakasi gani kwa Serikali kuingia ubia  na Sekta Binafsi (PPP) itakayowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa.

Serukamba amesema hayo leo Jumatatu Novemba 11, 2019, wakati akichangia katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mapendekezo ya Mwongozo

Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/2021.

Amesema wamekuwa wakitoa mifano ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuwa wameingia PPP lakini ukweli ni kwamba ni uongozi tu.

Serukamba amesema miradi ya PPP ni ile ambayo sekta binafsi inaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi na kisha kugawana faida.

Amesema kama Serikali haina fedha kwa sababu inatekeleza katika mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere basi itafute wabia watakaotekeleza katika miradi mingine ya umeme.

“Umeme ni biashara. Tuzalishe tutauza nje ya nchi. Kama hatuwezi kufanya kwa wakati mmoja (miradi) lazima tufanye kwa PPP,” amesema.

Ametoa mfano wa barabara ya haraka ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma inaweza kujengwa kwa PPP.

Amesema ingawa kuna watu ambao wanasema kuwa kwa sababu Reli ya Kisasa inajengwa hakuna haja ya barabara hiyo lakini bado kuna haja ya kufanya hivyo.

Amesema mradi wa Gesi Asilia (LNG), Mchuchuma na Mwangaruka ingeweza kuzalisha zaidi ya Sh40 bilioni ambazo zitaingia katika uchumi.