Mbunge CCM asema barabara ya Mvumi Dodoma imeoza, Serikali yamjibu

Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde akiuliza swali katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 18 wa Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema itaanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami  barabara ya Mvumi Mission mkoani Dodoma ambako kuna hospitali maarufu ya kutibu matatizo ya macho.

Dodoma. Mbunge wa Mtera (CCM), nchini Tanzania, Livingstone Lusinde amesema hali ya barabara kuelekea hospitali ya Mvumi imeoza hivyo ni hatari kwa maisha ya watu.

Katika swali la nyongeza bungeni leo Jumanne Januari 28,2020, Lusinde amesema umuhimu wa hospitali ya Mvumi Mission unapotea na uzuri wa hospitali hiyo unakosekana kama hakutakuwa na barabara ya lami.

"Hata hiyo kilomita moja wanayosema imeanza kujengwa naona wamemdanganya Waziri, hakuna kitu, hali ni mbaya hasa kwa akina mama wanaohitaji huduma za hospitali hiyo na barabara nyingi nchi nzima zimeoza kabisa, nini mpango wa serikali katika eneo hilo," amehoji Lusinde.

Mvumi ndiyo hospitali kongwe kwa ajili ya wenye matatizo ya macho na kwa sasa ndiyo hospitali teule ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, John Malecela ambaye aliwahi kuongoza jimbo hilo ni mwenyeji wa Mvumi makazi yao yakiwa karibu na Lusinde maarufu Kibajaji.

Katika majibu ya serikali, Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema kutokana na umuhimu wa hospitali hiyo, wameanza maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara hiyo.

Waitara amesema kwa kuanza wamepanga kujenga barabara hiyo kwa urefu wa kilomita moja kazi itakayokamilika Agosti 2020.