Mbunge CCM asema wahudumu wa ATCL hawana mvuto kwa wateja

Mbunge wa Kigoma Kusini nchini Tanzania (CCM) Husna Mwilima

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini nchini Tanzania (CCM) Husna Mwilima amesema wahudumu wa ndege wanaoajiriwa na Shirika la Ndege Nchini (ATCL) hawana mvuto kwa wateja.

Mwilima ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 7, 2019 wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo bungeni jijini Dodoma.

Mwilima amempongeza Rais John Magufuli kwa kutimiza ahadi yake ya kuifufua ATCL na kuwataka mawaziri pia kutimiza ahadi zao.

“Mheshimiwa waziri mimi nataka nitanie kidogo hizi ndege zetu zinafanya vizuri sana lakini mle ndani hebu tuangalie tunaowaajiri. Wale maair hostess (wahudumu) hata ukimuita mle ndani akigeuka abiria anaona kweli tuna maair hostess mle ndani,”amesema na kuongeza:

“Sijui mnatumia vigezo gani? Unakuta air hostess mfupi, hana mvuto wa kuifanya ndege zetu zionekane. Leo mimi hapa nimezeeka na miaka 50 na ukiniweka…”amesema kabla ya kukatishwa na utaratibu uliombwa na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma.

Musukuma amesema huo ni ubaguzi na kwamba kuna wengine wanazaa watoto ambao hawana maumbo kama anayoyasema mbunge huyo.

Akiendelea kuchangia Mwilima amesema sifa ya mhudumu wa ndege ni lazima awe mrefu na amenyooka akiwa mwanaume ama mwanamke na kuomba jambo hilo lizingatiwe.