Mbunge CCM ataka gereza lenye watu maalumu likarabatiwe

Mbunge wa Temeke (CCM), Abdallah Mtolea

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema italifanyia marekebisho Gereza la Keko jijini Dar es Salaam. Uamuzi huo unatokana na Mbunge wa Temeke (CCM), Abdallah Mtolea kudai gereza hilo limekuwa katikia hali mbaya.

Dodoma. Mbunge wa Temeke (CCM), Abdallah Mtolea ameiomba Serikali ya Tanzania kulifanyia marekebisho gereza la Keko lililoko jijini Dar es Salaam kwa kuwa linachukua watu maarufu wenye kesi kubwa kubwa.

Mtolea ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatano Januari 29, 2020 wakati akiuliza swali la nyongeza akisema gereza hilo lina upekee kwani hupokea wahalifu wa ‘VIP’.

Amesema licha ya Serikali ya Tanzania kulifanyia marekebisho madogo mwaka 2016, bado kuna tatizo kwa gereza hilo kutiririsha maji machafu katika makazi ya watu hususan kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

"Gereza hili hupokea wafungwa au mahabusu wa VIP kwa hiyo ilipaswa lifanyiwe ukarabati wa kutosha na kwa muda muafaka ili liwe katika ubora unaotakiwa," amesema Mtolea.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amekiri gereza hilo linahitaji ukarabati na Serikali itafanya ukarabati wakati bajeti itakaporuhusu.