Mbunge CCM ataka mabadiliko sheria ya ndoa, mirathi

Mbunge wa Mpwapwa George Lubeleje akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha muswada wa sheria ya marekebiusho ya sheria mbalimbali (Na.8) wa mwaka 2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi  kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya mirathi na ndoa.

Dodoma. Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi  kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya mirathi na ndoa.

Lubeleje ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 28, 2020 bungeni mjini Dodoma wakati akichangia muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 8 wa mwaka 2019.

Muswaada huo umewasilishwa bungeni na Profesa Kilangi aliyeliomba Bunge kuupitisha kwa kuwa unagusa maeneo tofauti ya sheria.

"Mimi naomba ije hapa miswada ambayo inagusa mambo tunayoyalalamikia ya ndoa na mirathi. Huwezi kuleta sheria ya mtoto hapa halafu ukaacha sheria za lazima,” amesema Lubeleje.

Amesema katika marekebisho yaliyopo katika muswada huo, Serikali inataka kuondoa utaratibu uliokuwepo ambao mdai na mdaiwa wanaweza kukubaliana nje ya mahakama ili waendelee kulipana kwa utaratibu, kwamba sasa inakuwa jinai.

Naye mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi ameitaka Serikali kuangalia utozaji faini kwa wavuvi haramu.

Mkundi anasema kiwango cha faini ya Sh10 milioni kwa mtu atakayekamatwa akivua bila utaratibu kitawapeleka wengi gerezani.

Katika muswada huo imependekezwa kuwa mtu akibainika kuhusika katika uvuvi haramu adhabu  ni Sh10 milioni au kifungo cha miaka miwili.