Mbunge Chadema aahidi kugawa fedha kwa usawa

Sunday December 1 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja anayewania uweka hazina wa chama hicho Kanda ya Kati amesema atagawa fedha zitakazopatikana kwa usawa katika majimbo 31.

Kanda ya Kati ya chama hicho ni mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba Mosi,  2019 wakati akiomba kura katika uchaguzi wa viongozi wa Kanda hiyo.

Amesema atawajibika kutafuta fedha kwa ajili ya  operesheni za Chadema na  atakuwa tayari kutoa fedha mfukoni mwake wakati akisubiri ruzuku kwa ajili ya uendeshaji shughuli za kanda hiyo.

"Nimekuwa mwandishi wa habari nina mawasiliano  ndani na nje ya nchi naomba mnitume, niwatumikie," amesema akisisitiza kuwa hatakuwa mtunza fedha pekee bali mtafuta fedha kwa kubuni vyanzo vya mapato.

Tully Kiwanga anayetetea nafasi hiyo, amesema endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo kwa mara nyingine atahakikisha wanajenga ofisi ya chama kanda ya kati kwa kutumia nguvu za wanachama.

Advertisement

Amesema mwaka 2020 atatimiza miaka tisa tangu ajiunge na Chadema na kwamba amekuwa mwanachama mwaminifu katika kipindi chote.

Advertisement