Mbunge Chadema ahoji agizo la Magufuli kuhusu wacheza pool table muda wa wakazi

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema),  Grace Tendega ameitaka Serikali ya Tanzania kueleza hadi leo Ijumaa Februari 7, 2020 kuna kambi ngapi za watu waliokamatwa wakicheza mchezo wa pool table wakati wa kazi.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema),  Grace Tendega ameitaka Serikali ya Tanzania kueleza hadi leo Ijumaa Februari 7, 2020 kuna kambi ngapi za watu waliokamatwa wakicheza mchezo wa pool table wakati wa kazi.

Grace amehoji suala hilo leo bungeni mjini Dodoma akirejea kauli ya Rais John Magufuli ya Machi 15, 2016 wakati akiwaapisha wakuu wa Mikoa ambapo aliagiza vijana wanaocheza mchezo huo kukamatwa, kupelekwa kambini kulima.

“Serikali imeandaa kambi ngapi na imewekaje huduma za kujikimu kwa vijana hao watakapokuwa wakiendelea na shughuli za kilimo wakati wakisubiri mavuno,” amesema Grace.

Mbunge huyo pia amehoji  mpango mkakati wa Serikali kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

“Je,  Serikali imefanya sensa kujua ni vijana wangapi wanaofanya kazi usiku na kupumuzika mchana au mchana na kupumzika usiku ili kubaini wazururaji wa mchana na wanaocheza pool table mchana kwa sababu ya kukosa ajira,” amesema.

Akijibu swali hilo naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde amesema agizo la Magufuli lililenga kusisitiza na kuimarisha dhana na tabia ya kila mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye.

Amesema katika kuhakikisha vijana wanashiriki shughuli za kiuchumi, Serikali kupitia tawala za Mikoa na Wilaya imetenga maeneo maalum ya uzalishaji mali kwa vijana.

Amesema ekari 217,882.36 zimeelekezwa katika kukidhi mahitaji ya shughuli za kilimo, ufugaji, viwanda na biashara ndogo.

Mavunde amesema katika kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuwajengea vijana ujuzi kupitia programu ya kukuza ujuzi.

“Kwa mwaka huu wa fedha Serikali inatekeleza mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi na vijana 49,265 watanufaika,” amesema.

Amesema wameweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ili kuwavutia wawekezaji wakubwa wa sekta zenye uwezo wa kuzalisha ajira hususani kilimo, ufugaji, madini na viwanda.

Kuhusu idadi vijana wanaofanya kazi usiku na mchana, Mavunde amesema Serikali imelipokea wazo hilo, “”suala hili  litawasilishwa katika mamlaka ya takwimu ili lizingatiwe katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.”