Mbunge Chadema azua jambo bungeni

Friday November 8 2019

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani,  Kangi Lugola amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwachukulia hatua watu aliodai wanaotoa kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa amani akiwemo mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda.

Lugola ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 baada ya Mwakagenda katika kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Dodoma kutamka kuwa  amemfukuza mpangaji wake kwenye nyumba kwa sababu  haoni umuhimu wa kushirikiana naye.

Mwakagenda alitoa kauli hiyo baada ya kupewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa. Hata hivyo alipotamka maneno hayo aliketi.

Baada ya Mwakagenda kueleza hayo mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga aliomba mwongozo na kuhusisha  uamuzi wa Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, na vurugu zinazojitokeza.

Huku akimtaja Mwakagenda, amesema mbunge huyo amemuondoa mpangaji wake na jana aliona wananchi wamefyeka shamba la msimamizi wa uchaguzi wilayani Butiama.

Mlinga amesema Chadema kimekuwa kikisusa kushiriki chaguzi mbalimbali na akataka kujua hatua ambazo Serikali itazichukua dhidi ya chama hicho.

Advertisement

Mwongozo kama huo pia uliombwa na mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa.

Akijibu miongozo hiyo baada ya kupewa nafasi na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Waziri huyo wa Mambo ya Ndani amesema Serikali haitanyamaza wala kutochukua hatua kwa vitendo vinavyohatarisha usalama na mali za wananchi.

Amesema polisi wamejipanga kuchukua hatua kwa mtu yeyote, vikundi ama vyama vya siasa  vitakavyofanya fujo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Nina taarifa chama kimoja kimejitoa katika uchaguzi ni imani yangu kuwa chama hiki kinaweza kikawa na mpango wa kufanya fujo ya kuvuruga amani na usalama wa nchi hii,” amesema Lugola.

Amesema hakutakuwa na nafasi yoyote ya vyama vya siasa kufanya mipango inayovunja na kuhatarisha imani ya nchi.

Amesema waanze kumchukulia hatua mbunge aliyeanza kuonyesha viashiria vya kuvunja amani

Advertisement