Mbunge Chadema kutimkia NCCR Mageuzi akimaliza ubunge

Mbunge wa Moshi Vijijini(Chadema), Anthony Komu

Muktasari:

Mbunge wa Moshi Vijijini(Chadema) Anthony Komu ametangaza kujivua uanachama kwa sababu ya kukatishwa tamaa na tuhuma za usaliti zinazoendelea kutolewa dhidi yake
Hata hivyo Komu amesema ataondoka rasmi baada ya kumaliza muda wake wa ubunge kwa kuwa bado atahitaji ushirikiano wa chama hicho jimboni

Dar es Salaam. Mbunge wa Moshi Vijijini(Chadema), Anthony Komu ametangaza rasmi kujivua uanachama kwa sababu ya kukatishwa tamaa na tuhuma za usaliti zinazomkabili kwa muda mrefu.
Hata hivyo, amesena ataondoka rasmi baada ya kumaliza muda wake wa ubunge kwa kuwa bado atahitaji ushirikiano wa chama hicho jimboni kabla ya kumaliza muda wake.
Akizungumza na wanahabari leo Machi 29,2020 jijini Dar es salaam, Komu amesema amechukua uamuzi huo baada ya kusikitishwa na uongozi wa chama hicho kutosahihisha au kufafanua tuhuma za usaliti zilizosababisha mbengu ya chuki kukomaa ndani ya chama.
"Nimeomba kukutana nanyi(wanahabari) ili kuweka bayana mwelekeo wangu wa kisiasa, kwa sababu ya mijadala ya muda mrefu juu ya mwelekeo wangu wa baadaye," amesema Komu.
Komu anakuwa mbunge wa tisa kati ya 35 waliojivua uanachama kwa madai mbalimbali ya kukosekana kwa demokrasia ndani ya chama au kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.
Licha ya kukiri kutofautiana na viongozi wenzake, lakini tofauti za kimitazamo zimemfanya aonekane muasi.
"Hatua hiyo ilisababisha kutoaminika hata pale ambapo ningeweza kutoa mchango wangu katika ujenzi wa chama chetu," amesema Komu aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Fedha wa Chadema.
Komu ametaja baadhi ya visa na tuhuma za usaliti alizokutana nazo licha ya kuwa mstari wa mbele katika hatua na matukio mbalimbali yaliyokijenga chama hicho hadi sasa.
Baadhi ya madai aliyoshambuliwa na wanachama wenzake ni pamoja na kupanga njama za kumuua Tundu Lissu, kwa kushirikiana na mtanzania aliyempokea Ubelgiji kwa matibabu.
Katika hotuba yake iliyotanguliwa na tahadhali za maambukizi ya virusi vya corona(COVID 19) nchini, Komu ameeleza namna alivyoshiriki kujenga mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, akiimarisha upinzani kupitia NCCR Mageuzi  kabla ya kuhamia Chadema.
"Msimamo huu naomba upokelewe kwa mtazamo chanya Chadema, utasaidia kuondoa majungu yanayoendelea, eti nataka nihakikishiwe kurudi nafasi ya ukurugenzi wa fedha, kurudi jimboni, eti kupindua nafasi ya mwenyekiti wetu," amesema Komu.