Mbunge Kubenea asema haondoki Chadema

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea

Muktasari:

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hawezi kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hawezi kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Amesema  hawezi kuondoka Chadema  na kumfuata Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu aliyetangaza kuwa ataondoka katika chama hicho na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

Machi 29, 2020, Komu alitangaza kuwa hatakuwa mwanachama wa Chadema baada ya kumaliza muda wake wa ubunge kutokana na  kuchoshwa na tuhuma za usaliti zinazomkabili kwa muda mrefu bila uongozi kutoa ufafanuzi jambo linalosababishwa atengwe.

Kubenea pia ni miongoni mwa wabunge walioanza kutajwa kuondoka ndani ya chama hicho hususani baada ya kuondoka Komu ambaye waliadhibiwa pamoja Oktoba 2018 baada ya kukiri kosa la kupanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

“Baada ya Komu kuondoka kumeibuka maneno mengi, nikitajwa niko njiani kufuata naye. Nikiri kwamba Komu si mbunge mwenzangu tu, ni ndugu  na rafiki yangu kabisa lakini urafiki huo haunifanyi kila anachokifanya Komu na mimi pia nikifanye.”

“Lakini pia inawezekana anachofanya Komu na mie nikakifanya. Kwa sababu ya urafiki huo. Lakini hizo ramli wanazopiga waziache, mimi bado mbunge wa Chadema kutoka jimbo la Ubungo. Nadhani nahitaji kuwatumikia wananchi wangu mpaka muda wangu utakapomalizika. Watu waache ramli muda ukifika tutazungumza haya mambo,” amesema Kubenea.

Kubenea alitakiwa kujibu maswali kadhaa, ikiwamo suala la kuonekana kujitenga na shughuli za Chadema,kubomoka kwa kambi yake na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye aliyerejea CCM pamoja na kwa nini wanachama wenzake wametuhumu kuondoka.

Kuhusu kujitenga Kubenea amesema, “nimeshiriki kwenye michango, hata gerezani nilikwenda, nimekuwa mara kadhaa kwenye kesi za mahakamani, hata Mwenyekiti wetu Mbowe alipopata matatizo ya kuondolewa vitu nje katika ukumbi wa Billcanass, ofisi yake ilihamia hapa Mwanahalisi  yote kupigania uhuru wa vyombo vya habari.”

“Kuhusu kusemwa kwamba naondoka, hili nimesemwa sana watu wame-tweet sana, wametabiri sana lakini bado nipo, muda ukifika tutazungumza haya mambo.”

Kubenea amesema kundi linalodai kuwa ni usaliti  halifahamu na amekuwa akifanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa chama hicho.