VIDEO: Mbunge Ulega awapa CCM Sh10 milioni, vifaa vya uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega ametoa Sh10 milioni na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa katika jimbo hilo.

Mkuranga. Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega ametoa Sh10 milioni na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa katika jimbo hilo.

Uchaguzi huo utafanyika Novemba 24, 2019.

Ametoa fedha na vifaa hizo zikiwemo spika 25  katika mkutano mkuu maalum wa CCM wilaya ya Mkuranga uliohudhuriwa na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa,  Kanali mstaafu Ngemela Lubinga.

Ulega ambaye ni naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ametoa spika hizo zenye nyimbo mbalimbali za chama hicho tawala kwa maelezo kuwa zitatumika katika kampeni hizo.

"Spika hizi unaweza kuzichaji katika umeme, kutumia betri na sola. Zitapelekwa katika kata zote 25 za jimbo hili la Mkuranga," amesema Ulega.

Naibu waziri huyo pia ametoa  bendera 1,380 za chama hicho, kadi 3000 za uanachama, jezi na mipira 18.

"Pia ninatoa Sh10 milioni kwa ajili ya kutumika katika uchaguzi huu na ninakikabidhi chama wilaya. Fedha hizi nataka ziende katika matawi yote 247," amesema Ulega.

Katika mkutano mkuu huo wabunge wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu na Subira Mgalu ambaye pia ni naibu Waziri wa Nishati kila mmoja ametoa Sh500,000.