Mbunge mwingine wa CUF ahamia CCM Zanzibar

Muktasari:

Mbunge wa Ole (CUF), Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba Zanzibar, Juma Hamad Omari amejiuzulu nafasi zake na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM)

Dar es Salaam. Mbunge wa Ole (CUF), Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba Zanzibar, Juma Hamad Omari amejiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho na kuomba kujiunga na CCM.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Machi 3, 2020 imesema kuwa mbunge huyo amepokelewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Omari akiwa ameambatana na wanachama wa CUF na ACT-Wazalendo 564 wamepokelewa katika mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Chakechake.
Mbunge huyo anahamia CCM ikiwa ni siku moja tangu mbunge mwingine wa CUF visiwani humo kutangaza kujivua uanachama na kujiunga na CCM.
Jana Jumatatu Mbunge wa Wawi (CUF), Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Juma Ngwali amejivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM.