VIDEO: Mbunge wa Chadema aachiwa baada ya kusota rumande

Katavi. Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Rhoda Kunchela ameachiliwa huru leo Februari 26, 2020 saa 7:30 mchana, baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mpanda mjini kwa siku moja.

Mara ya kwanza Rhoda alikamatwa Januari 9, 2020 akituhumiwa kufanya mkutano bila kibali na kuachiwa siku hiyohiyo saa 5 usiku kwa dhamana na kutakiwa kuripoti polisi Februari 11, 2020 ili kujua kama kesi yake itapelekwa mahakamani jambo ambalo inadaiwa hakufanya.

Rhoda alikamatwa tena Februari 25, 2020 saa 5:00 asubuhi baada ya kwenda kuripoti kituo cha polisi.

"Nilikamatwa na kunyimwa dhamana wakati nina uthibitisho wa cheti cha daktari, nimeacha kunyonyesha mwanangu wa umri mwaka mmoja wakadai watanishikilia hadi jalada la kesi likamilike,"

"Kwa sasa wameniachia huru kwa sababu mtuhumiwa mmoja   Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mpanda mjini, Boniphace Mganyasi, hakuripoti polisi," amesema Rhoda.

"Nilishindwa kuripoti siku hiyo kwa sababu nilirudi bungeni Dodoma na baadaye nilipata maradhi ni vyema wangenipeleka mahakamani leo ndiyo napewa dhamana na kutakiwa kuripoti Februari 28, 2020 saa 5:00 asubuhi huu siyo utu," amesema.

Katibu Mwenezi wa Chadema Mpanda mjini, Hamisa Korongo Mongomongo amesema amesikitishwa na kitendo hicho akieleza kuwa ni cha unyanyasaji.

"Mheshimiwa aliandika barua na kupokelewa na afisa upelelezi kuwa atakuwa nje ya mkoa na akaruhusiwa kwenda bungeni na kuelezwa kuwa atapewa taarifa atakapohitajika, amerudi amekamatwa tena alichofanyiwa ni kitendo cha udhalilishaji,"amesema Hamisa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ronald Makona amesema hana taarifa kuhusu taarifa hizo.

"Mwandishi sikuwepo na sasa natoka kwenye kikao, ngoja nifuatilie nitakupa taarifa baadaye," amesema Makona.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi