Mbunge wa Chadema ahoji kuhusu vitambulisho vya wamachinga

Mbunge wa viti Maalum (Chadema) Aidan Kenani akichangia mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum(Chadema) nchini Tanzania, Aidani Kanani ametaka Serikali kueleza ina mkakati gani endelevu wa kutoa vitambulisho vya wamachinga.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum(Chadema), Aidani Kanani ameitaka Serikali kuwaambia Watanzania ina mkakati gani endelevu wa kutoa vitambulisho vya wamachinga.

Akichangia Ofisi ya Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Aidani amesema bado Serikali haijasema kuwa vitambulisho hivyo vimezalisha kiasi gani cha fedha.

“Inaleta maswali mengi sana, vitambulisho vimepatikana kiasi gani, kuna mkakati gani endelevu? Amehoji mbunge huyo.

Amesema ni vyema Serikali ikianzisha jambo ikasema hitimisho lake linakuwaje ili kuondoa maswali mengi yanayotoka kwa wananchi.

Pia amehoji watendaji waliozuia na kufunga ofisi wakati wa urejeshaji wa fomu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana wangapi wamechukuliwa hatua.

“Viongozi katika ni wangapi wamechukuliwa hatua? Huko ni hali mbaya. Hali ni mbaya sana ingawa wenyeviti wote ni CCM lakini hawafanyi vizuri huko. Wenyeviti wanatakiwa kutokana na wananchi kwa kuchaguliwa,”amesema.