VIDEO: Mbunge wa Rufiji afikisha kilio cha mafuriko bungeni

Mbunge wa Rufiji nchini Tanzania (CCM),  Mohamed Mchengerwa

Muktasari:

  • Mbunge wa Rufiji nchini Tanzania,  Mohamed Mchengerwa amefikisha kilio cha mafuriko yaliyotokea kwenye jimbo lake na kusababisha watu zaidi 20,000 kukosa makazi na chakula.

Dodoma. Mbunge wa Rufiji nchini Tanzania (CCM),  Mohamed Mchengerwa amehoji hatua zinazochukuliwa na Bunge kuwaangalia watu waliokumbwa na maafa ya mafuriko kwenye wilaya hiyo ambao ni kati ya 20,000 hadi 50,000.


Mchengerwa amewasilisha kilio hicho leo Jumanne Machi 31 2020 mara baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa taarifa ya utaratibu waliouweka katika kujikinga na virusi vya corona.


Mbunge huyo amesema nchi yote imekumbwa na mafuriko yaliyosababisha maumivu kwa wanyama, binadamu na miundombinu na vitu vingine vingi.


Hata hivyo, amesema pamoja na kwamba mafuriko yamejitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini lakini yapo yamesababisha maumivu makubwa ikiwemo Rufiji.


“Wananchi zaidi ya 20,000 hadi 50,000 wamekuwa hawana maeneo ya kuishi, vyakula na wamekuwa wakipambana kuokoa maisha yao. Je kama Bunge tunachukua hatua gani kuwaangalia wananchi hao wanyonge ambao pia wako katika maafa ya mafuriko? Amehoji.
Akijibu Spika Ndugai amesema Serikali imepata ujumbe huo na imeendelea kuchukua hatua.


Hata hivyo, amesema  wakati fulani wataiomba Serikali iwape taarifa kuhusu mambo yanayoendelea wilayani humo na hivyo kujua nafasi ya Watanzania wote kuwasaidia