Mbwembwe za Kangi Lugola zilivyoyeyuka ndani ya siku 571

Sunday January 26 2020

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

“Na ninataka niwaambie Watanzania, siku mkibeza juhudi zinazofanywa, amani, usalama ukakatika, fedha zote Rais atazielekeza kununua risasi na mabomu kwa ajili ya kulinda nchi, matokeo yake hatutajenga hospitali, shule, watu hawatolima na matokeo yake nchi itakuwa masikini. Magufuli oyee!”

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya mwisho ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliyoitoa Januari 23 wakati wa uzinduzi wa nyumba za askari magereza zilizoko Ukonga jijini Dar es Salaam, kwani baada ya Rais John Magufuli kusimama jukwaani alitangaza kumfukuza kazi.

Mbali na Lugola wengine walioondolewa ni Kamishna Jenerali wa Zimamoto, Thobias Andengenye aliyeenguliwa katika nafasi hiyo wakidaiwa kushiriki kuandaa mkataba ambao Rais Magufuli alisema ni wa hovyo.

Hata hivyo, Rais Magufuli alimpongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kwa kujiuzulu mapema kabla sakata hilo halijawekwa wazi.

“Nitaendelea kuwapenda lakini kwenye nafasi zenu hapana. Watanzania mmenichagua kusimamia haki na utendaji kazi ndani ya Serikali ili kila fedha ya Watanzania ikatumike kwa mujibu wa sheria,” alisema Rais Magufuli.

“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni. Mradi huo umesainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto.”

Advertisement

“Haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge. Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda katika majadiliano na kulipwa Dola 800 za posho ya vikao,” alisema Rais Magufuli na kubainisha kuwa hata tiketi za ndege walilipiwa.

Alisema kwamba mkataba huo ni wa hovyo kwa sababu ili kuuvunja yaliyoanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.

“Lugola nampenda sana ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari pamoja na mwili na ukubwa wake lakini katika hili hapana. Nilitegemea hata hapa sitamkuta, nasema kwa dhati.

“Andengenye nampenda sana ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa.

Hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu namna hii. Yanayokwenda kununuliwa katika mkataba ni ya hovyo.”

Ameongeza, “nampongeza Kingu kwa kuwajibika na hii imempa heshima kwamba angalau ametambua, inawezekana haya hakuyafanya yeye lakini kwa kuwa yeye ni katibu mkuu amewajibika kwa hilo, nampongeza na nitaendelea kumheshimu.”

Kangi Alphaxard Lugola maarufu kwa jina la Ninja aliyezaliwa Mei 25, 1963 amekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa 26 tangu Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961, atakumbukwa kwa siasa zake za majigambo na mizaha hasa kucheza muziki anapokuwa kwenye matukio mbalimbali ya kiserikali.

Alikuwa mbunge wa Jimbo la Mwibara mkoani Mara tangu mwaka 2010. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Julai Mosi, 2018 akimrithi Mwigulu Nchemba aliyeenguliwa katika nafasi hiyo na Rais Magufuli.

Kabla ya kuwa waziri, Lugola alionekana kuwa mbunge mchachari aliyekuwa tayari hata kuikosoa Serikali akiwa bungeni.

Miongoni mwa hotuba zake iliyoibua vicheko bungeni ni ile aliyoitoa Novemba 28, 2014 alipoomba kuvaa kofia ya ki-Ninja ili asiwaonee haya mawaziri waliokuwa wakitumiwa, wakati akichangia ripoti ya Tegeta Escrow.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kama kanuni zinaruhusu naomba uniruhusu nivae ki- Ninja ili nisiwatazame usoni,” alisema Lugola na kuzua vicheko kutoka kwa wabunge.

Hata hivyo, aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Idd Azzan Zungu hakumruhusu kuvaa kofia hiyo.

Aliendelea; “ahadi Na. 8 ya mwana CCM inasema naomba wana CCM wenzangu mnielewe, ‘nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ibara ya tano inaonyesha madhumuni na malengo ya CCM, nimepitia malengo yote, hakuna mahali ambako kanuni inasema CCM tutalinda wezi.”

Kama hiyo haitoshi, Lugola pia alimwomba Mwenyekiti wa Bunge avae sare za CCM lakini pia alikataliwa.

Mchango mwingine uliozua mjadala ni ule alioutoa Juni 29, 2016 wakati akichangia muswada wa marekebisho ya Sheria ya ununuzi wa Umma.

Akichangia pia bajeti ya Wizara ya Maji Mei 11, 2017 alipotangaza kuzunguka nchi nzima kama itapitishwa bila kuwekewa nyongeza ya tozo ya maji.

“Nataka niwaambie wabunge wenzangu atakayepitisha bajeti hii kwa ‘ndiyo ndiyo ndiyo wakati haijaongezwa tozo ya Sh50 niko tayari na mimi kuanzisha mwenge wa sauti, nitachukua kwenye hansard suti za wabunge za ndiyo nitazikimbiza nchi nzima nitawaambia kina mama, sikilizeni wabunge wanavyowasaliti na ninyi hamna maji,” alisema.

Alipopewa uwaziri

Alipoteuliwa kuwa Waziri Lugola akabadilika kuanza kuisimea Serikali. Kwanza mtindo wake wa mavazi ukabadilika.

Wakati mtangulizi wake, Mwigulu Nchemba alikuwa akipenda zaidi kuvaa skafu ya bendera ya Taifa shingoni, yeye akawa akivaa kaunda suti zenye mifuko ya bendera za Taifa kwa upande wa kulia na kushoto.

Kama hiyo haitoshi, Waziri Lugola alikuwa akitembea na ilani ya CCM katika mikutano yake.

Julai 6, 2018 ikiwa ni siku sita tu baada ya kuteuliwa, Lugola alimfukuza kikaoni aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa kwa kuchelewa kufika kwenye kikao hicho kwa dakika moja.

Kabla ya kikao hicho, Lugola alitoa agizo kwamba ikifika saa 5:00 mlango wa ukumbi waliokuwa wakifanyia mikutano ufungwe, muda ulipowadia mlango huo ulifungwa kama alivyoagiza lakini dakika moja baadaye (saa 5:01) mlango ulifunguliwa ili Dk Malewa aingie. Hata hivyo, mara baada ya kuingia, Lugola akahoji kwa nini amefunguliwa mlango? Licha ya Dk Malewa kuomba msamaha, Lugola aligoma na kumfukuza kwenye kikao hicho.

Lugola na vyama vya siasa

Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani anayesimamia Jeshi la Polisi, Lugola alionekana kuwa mchungu kwa vyama vya upinzani akizuia haki ya vyama hivyo kufanya mikutano na maandamano kwa mujibu wa sheria.

Akiwa mjini Zanzibar Machi 25, Lugola alihutubia mkutano wa hadhara na kutoa onyo kwa wanasiasa aliodai kuwa wanaunda magenge ya uhalifu.

“Safari hii hatuangalii sura ya mtu, rangi ya mtu, kiwango cha msitu wa ndevu alichonacho mtu, wala kiwango cha sharubu alichonacho na sana sana ukamataji wetu utaanzia kwenye msitu wa ndevu pamoja na sharubu kuhakikisha kwamba tunawashughulikia,” alisema Lugola.

Aliendelea, “Kuna baadhi ya watu sisi tunaamini kuwa ni vyama vya siasa, lakini tumegundua ni magenge ya wanasiasa ambao wamepanga mipango ya kufanya mikutano ya hadhara iliyozuiwa, narudia kufanya mikutano ya hadhara na maandamano yaliyozuiwa,” alisema.

Suala la kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano limekuwa likilalamikiwa na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia kwa kuwa linakwenda kinyume cha sheria na Katiba.

Licha ya malalamiko hayo, Lugola alikanusha kuyasikia alipokuwa akizindua ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dodoma Septemba 26, 2019.

Alisema sheria inawataka watu wanaotaka kukusanyika kulipa taarifa Jeshi la Polisi, wakiona kimya wanaendelea ila wakipewa barua ya zuio wanatakiwa kusitisha shughuli hizo na kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo.

Alisema wanaolalamika na kuanza kufanya wanachokitaka wao lazima wakutane na mkono wa sheria kwani polisi iko imara na hawawezi kuachwa.

Masihara

Mara nyingi Lugola akiwa kwenye mikutano ya hadhara alikuwa mwenye masihara akicheza ngoma au akishiriki kuimba nyimbo za wasanii wanaokuwapo kwenye hadhara hizo huku pia akitumia hotuba zake kumsifia Rais Magufuli.

Lakini sifa zote hizo hazijatosha kwa Rais Magufuli kumwengua kwenye uwaziri wake mchana kweupe na kuhitimisha safari yake ya kukaa katika kiti cha uwaziri kwa siku 570 kabla ya kuondoka.

Advertisement