Mchomelea vyuma aeleza alivyoshuhudia maandamano ya Chadema

Muktasari:

Shahidi wa pili katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake Freeman  Mbowe ameeleza kuwa alimuona akiwahamasisha wananchi kuendelea kuandamana.

Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake Freeman  Mbowe ameeleza kuwa alimuona akiwahamasisha wananchi kuendelea kuandamana.

Shahidi huyo Shaaban Abdallah (19) ambaye ni mchomelea vyuma eneo la Mkwajuni, ameeleza hayo leo Jumanne Mei 14, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, shahidi huyo amesema Februari 16, 2018 tangu majira ya asubuhi alikuwa eneo lake la kazi eneo la Kinondoni Mkwajuni.

Ameeleza kuwa siku hiyo majira ya saa 11:00  jioni akiwa amekwenda kununua vifaa vya kazi alifika dukani kwa mtu aliyemtaja kwa jina la moja la baba John kwa ajili ya kununua vifaa.

Amedai kuwa wakati wakiendelea na hesabu walisikia zogo kwa mbali, lakini hawakufuatilia baada ya muda waliona watu wengi katikati ya barabara wakitokea eneo la Morocco wakielekea Magomeni.

Shahidi huyo ameendelea kudai kuwa waandamanajii hao walionekana kuwa katika hali ya shari na walikuwa wakiimba, huku viongozi wao wakiwa mbele na aliweza kuwatambua  (Freeman) Mbowe, (Halima) Mdee, (John) Mnyika na (Ester) Matiko.

Ameeleza kuwa wakati wakiendelea kuwaangalia waandamanaji hao waliona gari la polisi likiwa nyuma yao likiwatangazia watawawanyike, lakini waliendelea kulisogelea na kuanza kurusha chupa za maji na mawe.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Jumatano Mei 15, 2019 itakapoendelea na ushahidi kwa upande wa mashtaka.

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent  Mashinji; Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu; Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika; Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee.

Wengine ni Ester Bulaya mbunge wa Bunda; Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini; Ester Matiko, mbunge wa Tarime Mjini; na John Heche, mbunge wa Tarime Vijijini.

Mbowe na viongozi wengine wanakabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, ikiwamo kuhamasisha wafuasi wao kutenda makossa na kufanya mkusanyiko usio halali.