Mchuano wa Shahidi na Kibatala kesi ya Mbowe

Muktasari:

Shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa picha alizopiga katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, hazionyeshi tarehe na muda uliopigwa.

Dar es Salaam. Shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa picha alizopiga katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, hazionyeshi tarehe na muda uliopigwa.

Ushahidi huo uliochukua saa saba kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi Saa 11:58 jioni.

Kibatala: Picha ulizopiga katika mkutano wa Chadema pale katika viwanja vya Buibui zinaonyesha tarehe na muda uliopigwa?

Shahidi: Hazionyeshi muda wala tarehe.

Kibatala: Tusaidie shahidi cheo cha Koplo ni cha ngapi katika Jeshi la Polisi?

Shahidi: Ni cheo cha tatu, kuna kuruta na constable.

Kibatala: Jana (juzi) uliileza mahakama kuwa umemaliza kidato cha nne, ukapata ufaulilu daraja la tatu pointi 24, bado pointi ngapi ufikie division four?

Shahidi: Sijui kwa sababu mifumo ya elimu inabadilika. Baada ya hapo nilienda kusoma Diploma ya Uandishi wa Habari.

Kibatala: Ni mshtakiwa yupi katika video uliochukua katika mkutano ule alitambulisha tarehe ya mkutano?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala:Unafahamu kama Freeman Mbowe alisema katika mkutano wa kufunga kampeni pale katika viwanja vya Buibui kuwa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini alilazimishwa kujiuzuru urais, je, hapo anakuwa ametenda kosa la jinai.

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Unafahamu aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia alijiuzuru kabla ya muda wake?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Katika video ile Mbowe alionekana akiuliza Magufuli ni nani, je, kuuliza hivyo ni kosa la Jinai.

Shahidi: Sifahamu kwa sababu mimi sio mpelelezi.

Kibatala: Kwani wewe shahidi una uhakika Freeman Mbowe anamfahamu Rais Magufuli ni nani?

Shahidi: Anamfahamu, Rais Magufuli ni figure (alama) ya nchi na hata Mbowe mwenyewe anamfahamu Rais Magufuli.

Kibatala: Ni nani aliyekuambia Mbowe anamfahamu Rais Magufuli?

Shahidi: Hakuna aliyeniambia ila kwa Mtanzania yeyote lazima amjue.

Kibatala: Katika video hiyo, Mbowe alisikika akisema Magufuli ni mwepesi kama karatasi tatizo liko wapi?

Shahidi: Inategemea kauli hiyo ameitoa katika muktadha gani ila kwangu kama ofisa wa Jeshi la Polisi niliona ni tatizo.

Kibatala: Hivi shahidi umeshawahi kumpima uzito Magufuli?

Shahidi: Sio kazi yangu.

Kibatala: Umewahi?

Shahidi: Sijawahi.

Kibatala: Katika video ile Mbowe alisema atadai haki, eleza atadai vipi kwa njia gani?

Shahidi: Sijui

Kibatala: Ni sahihi kuwa Mbowe ni mbunge wa Tanzania?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni sahihi kuwa Katiba ya Tanzania inaelekeza misingi ya Haki?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Sasa tatizo liko wapi mtu kuongoza mapambano kudai Haki?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ni nyaraka gani uliyoitoa kama kilelelezo mahakamani hapa kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoonyesha Chadema watafunga kampeni za uchaguzi?

Shahidi: Sifahamu kwa sababu mimi siyo mfanyakazi wa NEC.

Kibatala: Ni sahihi katika video ile Mbowe alisema hataki fujo, hataki watu wafanye fujo na wala hawata muua inzi wala kumdhuru mtu, bali wanataka amani.

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni sahihi maneno hayo Mbowe alikuwa anaongea wakati akiwa njiani anakwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni?

Shahidi: Hapana alikuwa katika mkutano wa Chadema katika viwanja vya Buibui, Mwananyamala.

Kibatala: Ulishawahi kuwapa mkanda huu wa video polisi au wapelelezi ili watumie kuwahoji washtakiwa polisi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Hufahamu vipi wakati katika ushahidi wako umetueleza kuwa wewe ndiyo ulitunza kamera na mikanda hii ya video? Kwa hiyo washtakiwa walihojiwa polisi kwa video nyingine?

Shahidi: Sifahamu kwa sababu mimi si mpelelezi katika kesi hii.

Kibatala: Ni sahihi kielelezo (kamera na mkanda miwili) ulikuwa unaitunza wewe na hakijawahi kutolewa sehemu yoyote hadi ulipokuja kuitoa mahakamani hapa?

Shahidi: Ni sahihi

Kibatala: Wakati unachukua matukio katika mkutano huo ulikuwa unapiga picha na video ukiwa juu ya gari au chini?

Shahidi: Katika gari la polisi ambalo ni gari la OCD na ndiyo lililonirudisha hadi Kituo cha Polisi Osyterbay.

Kibatala: OCD wako alikuwa anaitwa nani?

Shahidi: Afande Dotto.

Kibatala: Katika mkutano huo kulikuwa kuna waandishi wa habari wengine?

Shahidi: Ndio walikuwepo.

Kibatala: Katika video, tuliyoona, kuna sehemu imeonyesha watu wameshika fimbo, mawe au mikuki?

Shahidi: Sikuona

Kibatala: Ni sahihi eneo hilo la mkutano walikuwepo askari polisi?

Shahidi: Ndio, walikuwepo.

Kibatala: Katika video hiyo, kuna sehemu wafuasi wa Chadema walionekana wakiwashambulia polisi?

Shahidi: Hakuna

Kibatala: Je, katika video hiyo pia kuna sehemu wafuasi wakizomea polisi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Shahidi hapa Mahakamani kuna washtakiwa tisa, je, tukienda kuangalia ile video uliyoionyesha mahakamani jana (juzi), tutaona hawa washtakiwa wakiwa wanawarushia askari polisi chupa za maji na mawe.

Shahidi: Hakuna.

Kibatala: Ester Matiko alisema nini katika mkutano huo?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Je, Ester Matiko anaonekana katika video uliyorekodi wewe?

Shahidi: Hayupo katika video hiyo.

Kibatala: Shahidi unakumbuka Halima Mdee katika mkutano huo alisema nini?

Shahidi: Halima Mdee alisema kesho (yaani siku ya uchaguzi) wote wananchi wa Kinondoni tukamchinje Magufuli na vibaraka wake na kama mbwai na iwe mbwai.

Kibatala: Je, maneno hayo ni kosa?

Shahidi: Ni kosa la jinai kwa sababu maneno yake yanaleta chuki na kusababisha watu wamchukie Rais Magufuli na watendaji wake.

Kibatala: Kumchukia Rais ni kosa?

Shahidi: Sijui

Kibatala: Ulisikia Mdee anawaambia wananchi waende wakampige mawe Magufuli?

Kibatala: Kwani peoples power unaielewa ni kitu gani?

Shahidi: Mimi sifahamu

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Hivi kuichukia Serikali ni kosa?

Shahidi: Inategemea

Kibatala: Hebu tuambie unasema ulipoona fujo uliondoka eneo la mkutano, sasa ulitishika na nini? Tukienda kuagalia ile video tutaona wewe unashambuliwa?

Shahidi: Hatutaona.

Kibatala: Je, ulishambuliwa au haukushambuliwa?

Shahidi: Sikushambuliwa ila maeneo yaliyotamkwa baadhi ya viongozi katika mkutano huo, yalikuwa yanatishia uvunjifu wa amani.

Shahidi huyo pia alihojiwa na Jeremiah Mtobesya na Hekima Mwasipu. Awali, kabla ya shahidi huyo kuhojiwa, upande wa utetezi uliomba mahakama iwapatie mkanda wa video ili na wao waweze kuutumia katika kumhoji shahidi.

Kibatala, alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

“ Mheshimiwa hakimu, kwa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka baadhi ya maswali tunayomuuliza anasema hakumbuki labda mpaka turudie kuangalia mkanda wa video ulioonyonyeshwa jana (juzi)mahakamani hapa, tumeona ni vyema mahakama yako ikaturuhusu na kutupa mazingira wezeshi ya kwenda kuangalia tena video ile ili na sisi tuweze kumuuliza maswali yetu vizuri shahidi huyu.”

Hakimu Simba alikubaliana na upande wa utetezi wa kuruhusu video hiyo ionyeshwe tena katika ukumbi wa mikutano na mafunzo mahakamani hapo na kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 35.