Mchuano wa uspika, unaibu rasmi CCM

Muktasari:

Ni joto lingine ndani ya CCM. Joto hili ni la watia nia wa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika katika Bunge la 12.

Dodoma. Ni joto lingine ndani ya CCM. Joto hili ni la watia nia wa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika katika Bunge la 12.

Mbali na nafasi hizo, CCM pia imetangaza kuanza kutoa fomu kwa wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi za meya wa halmashauri ya jiji au manispaa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya.

Nafasi zote zimetangazwa jana na Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kwamba utoaji wa fomu hizo ulianza jana na utamalizika leo.

Mchakato wa kumpata Spika unakuja katika kipindi ambacho Bunge la 12 litakuwa na asilimia zaidi ya 95 ya wabunge wa CCM kutokana na vyama vya upinzani kupata wabunge wawili Tanzania bara na wanne Zanzibar, hata kama wakichaguliwa wabunge wa upinzani kutoka katika vyama hivyo, idadi yao haitazidi 15.

CCM baada ya Spika Pius Msekwa, haijawahi kuwa na Spika aliyekaa zaidi ya kipindi kimoja. Mrithi wa Msekwa, Samuel Sitta alikaa kipindi kimoja cha Bunge la Tisa.

Sitta alipojitokeza kuwania uspika wa Bunge la 10, Kamati Kuu ya CCM ilikata jina lake na ikaelezwa kipaumbele kilitolewa kwa Spika mwanamke na ndipo Anne Makinda, jina lake lilipitishwa na alichaguliwa na Bunge kuwa Spika.

Makinda ambaye kabla ya kuwa Spika alikuwa Naibu Spika wakati uspika wa Msekwa na Sitta, hakutaka kugombea tena baada ya Bunge la 10 kumaliza muda wake.

Sitta ndiye Spika pekee aliyeonekana kutoa nafasi kubwa kwa wabunge wa upinzani wakati wa mijadala bungeni, aliwabana mawaziri wajibu hoja kwa weledi na si blah blah.

Ndiye aliyeanzisha utamaduni wa Naibu Spika kuvaa joho, kwani wakati wa uspika wa Msekwa, Naibu Spika hakuwa anavaa joho zaidi ya Spika mwenyewe.

Pia, wakati wa Sitta, wabunge wachache walifungiwa kuhudhuria Bunge. Mbunge aliyefukuzwa bungeni alikuwa John Cheyo.

Wakati wa Bunge la 10 chini ya Makinda naye hakukuwa na matukio mengi ya wabunge kufungiwa au kutolewa bungeni. Mbunge aliyefukuzwa bungeni na Makinda alikuwa Zitto Kabwe. Wakati huo Naibu Spika alikuwa Job Ndugai.

Hata hivyo, wakati wa mchakato wa ndani ya CCM wa kumpata atakayewania kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la 11, majina zaidi ya 20 yalijitokeza kuwania nafasi hiyo.

Waliojitokeza ni Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Akson, Abdullah Ali Mwinyi, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Wengine ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Mahalu, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Mlaki, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dk Didas Massaburi, Dk George Nangale na Dk Medard Kalemani.

Wengine ni Julius Powertiller, Agnes Makune, Mwalika Watson, Muzamil Kalokola, Simon Rubugu, Veraikunda Urio, Gosbert Blandes, Banda Sonoko, Leonce Mulenda na Philip Marmo.

Hata hivyo, majina matatu ndiyo yalipenya kwenye Kamati Kuu ya CCM---Ndugai, Dk Tulia na Mwinyi. Ndugai ndiye alichaguliwa kuwa Spika na Dk Tulia alichaguliwa kuwa Naibu Spika.

Uongozi wa Ndugai ndani ya Bunge la 11, ndio Bunge lililowadhibiti zaidi wabunge wa upinzani na kanuni kadhaa za Bunge zilifanyiwa marekebisho katika kudhibiti nidhamu ya Bunge.

Bunge la 11 ndio lililoondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, ‘Bunge Live’, kuwavua ubunge wabunge wawili wa upinzani---Tundu Lissu na Joshua Nasari.

Pia, Bunge la 11 ndio Bunge lililojitenga na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwa tuhuma za kuliita Bunge dhaifu.

Nafasi za meya, mwenyekiti

CCM ambayo imeshinda nafasi nyingi za ubunge na udiwani ndiyo itakayounda halmashauri za jiji na manispaa na pia nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya.

Hivyo, joto la kuwania nafasi hizo limefunguliwa jana baada ya kutangazwa kuanza kutolewa fomu za kugombea nafasi hizo za uongozi kwenye Serikali za mitaa.

Halmashauri zilizokuwa chini ya upinzani sasa zitakuwa chini ya CCM, hivyo kuwa na fursa ya kutoa meya na wenyeviti wa hamlshauri.