ANTI BETTIE: Mchumba asiyekupenda achana naye, tafuta atakayekupenda

Nina mchumba ninampenda, naye nikimtizama machoni ananipenda, lakini kila siku ananiambia moyo wake haunitaki.

Nifanyeje?

Pole sana. Mtu anasikilizwa anachosema mdomoni na si machoni wala moyoni. Inawezekana anakupenda kweli kukutizama kutokana na ulivyo, lakini kimapenzi moyo wake haukukubali, kwanza amekusaidia kukueleza ukweli kuliko angejilazimisha ilihali moyo haukutaki bila shaka angekusumbua. Kwa kuwa hamjaachana, jipange taratibu kuachana naye na kutafuta mwenza ambaye atakukubali kwa mwili, macho na moyo na utafunga naye ndoa na kufanya naye maisha.

Ndoa ni maisha, kuna wanaosema muoane mtazoeana taratibu, hayo mambo yamepitwa na wakati hakuna kazi ngumu kama kuishi na mtu usiyempenda.

Usikimbie majukumu muhudumie mwenza wako

Umri wangu ni miaka 40, sijaoa ila nimedumu kwenye uchumba kwa miaka saba. Tatizo mchumba niliyenaye anapenda sana fedha kiasi nafikiria kumuacha nianze upya.

Naomba ushauri wako nifanyeje?

Inawezekana anakuomba fedha kukukomoa, huwezi kuishi kwenye uchumba kwa miaka saba halafu ukategemea huyo mwanamke atakuwa anakuhurumia na kufanya vitu vya maana, labda awe hafikirii mbali.

Halafu kupenda fedha maana yake nini, sikuelewi. Usikimbie majukumu mwanamke anatakiwa atafute fedha atumie na mwenza wake, unadhani usipomuwezesha wewe awezeshwe na nani? Hili neno wanaume mmekuwa mnajifariji nalo sana...Eti mwanamke anayekupenda hahitaji fedha.

Msijidanganye kama hakuombi wewe kuna anakoomba ili alinde penzi lako mpenda ‘vitonga’ ‘mteremko’ ‘kutereza’, tofauti na hapo lazima umuwezeshe bila kujali anafanya kazi na analipwa mshahara. Wanaume mjitafakari kwa hili, wewe ni mfano wa wengi wanaojitoa fahamu na kuwalalamikia wanawake kuwa wanapenda fedha.

Hujasema mnaishi wapi, ingekuwa kijijini vitu vingi hususani vyakula vipo ndani kwa sababu mlilima, mjini hali ni tofauti kila kitu cha kununua atafanya nini iwapo hatakuomba fedha?

Nakushauri ili asikuombe mtafutie shughuli ya kufanya ya kumuingizia kipato kama hana kazi, haijalishi ni shughuli gani hata ya kuuza genge kulingana na uwezo wenu wa kifedha, ingawa hilo pia halikuondolei nafasi yako kama mume ya kuhakikisha unatimiza majukumu ya msingi ya familia yanayohitaji fedha kwa asilimia kubwa.

!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

Mume bora anamjua anayeolewa

Habari Anti. Natamani kuolewa lakini nashindwa kutambua mwanaume sahihi wa kunioa ni yupi.

Nifanyeje?

Wewe ndiyo unajua unataka mume wa aina gani na unapenda au hupendi nini kwenye maisha yako ya ndoa. Ni ngumu mtu kukushauri mume bora ni yupi kwa sababu maisha hayafanani.

Lakini kuna vitu muhimu kama ucha Mungu, nidhamu binafsi na kwa watu wengine, kujali na muhimu zaidi kukupenda wewe kwa dhati.

Vingine huwa vinakuja baadaye huku wewe ukiwa injinia mkuu kuhakikisha ndoa yako inakuwa vile unavyotaka iwe.