Mchungaji Msigwa akosoa marekebisho ya sheria ya TLS

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha muswada wa sheria ya marekebiusho ya sheria mbalimbali (Na.8) wa mwaka 2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema lengo la Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni kutaka kuwadhibiti wanasheria wanaowasaidia wananchi.

Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema lengo la Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni kutaka kuwadhibiti wanasheria wanaowasaidia wananchi.

Msigwa ameeleza hayo leo Jumanne Januari 28, 2020 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 8 wa mwaka 2019.

Mchungaji Msigwa amesema wanahitaji wanasheria wasiingiliwe na mihimili mingine, “tunawahitaji wanasheria wasiingiliwe kwa kuwa wanawasaidia wananchi. Kuna ubaya gani wananchi wakijua haki zao au ndio mnadhani wakizijua watazidai. Kwanini tunataka kuwaminya wanasheria  katika majukumu yao?”

Januari 18, 2020 Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba iliwaalika wadau wa sheria kuchangia marekebisho katika Sheria ya TLS.

Katika marekebisho hayo, inapendekezwa  kufanyika mabadiliko ya sheria ya TLS pamoja na mabadiliko ya sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka ya wilaya) na Mamlaka za Miji.

Muswada huo yanajikita katika kuweka vikwazo kwa sifa ya uanachama wa Baraza la TLS, kuanzishwa kwa ukomo wa wajumbe wa baraza ambao utakuwa ni mihula miwili kila mwaka na kuanzishwa kwa utoaji wa hesabu na ripoti kuhusu TLS ambapo ripoti za ukaguzi, ripoti za mwaka na taarifa za mikutano mikuu zitatakiwa kupelekwa kwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria.

Mapendekezo mengine kwa sheria hiyo ni pamoja na kuanzishwa kanuni zitakazotawala kazi za mkutano mkuu wa TLS ambao sasa hautajumuisha wanachama wote bali mahudhurio yatakuwa ya uwakilishi.

Pia mapendekezo yanataka mikutano mikuu iwe inafanyika wiki ya pili ya Aprili ambapo kwa utaratibu wa sasa wajumbe 15 wa chama hicho wanaweza kuitisha mkutano mkuu, lakini mabadiliko yanataka theluthi moja ya wanachama wenye msimamo mmoja wakihusisha asilimia sawa ya uwakilishi kutoka kila kikundi cha ndani ya chama hicho wanaweza kudai mkutano huo.

Akizungumzia bungeni kuhusu mabadiliko hayo, mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda amesema marekebisho ya sheria yanayoweka utaratibu wa usuluhishi katika kesi za madai utapunguza mrundikano.