VIDEO: Mchungaji Rwakatare atoa ujumbe wa mwaka 2020

Muktasari:

  • Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, limezindua kongamano la siku nane kuanzia leo Desemba 8 hadi 15,2019, linalojulikana kama 'Shilo 2019' . Linawakutanisha waumini wa kanisa hilo kutoka nchi nzima ili kufanya maombi usiku na mchana, kuombea masuala mbalimbali.

Dar es Salaam. Mchungaji Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni nchini Tanzania, Gertrude Rwakatare ametoa ujumbe wa mwaka 2020 kwa waumini wa kanisa hilo na Watanzania, akisema ni mwaka wa mafanikio utakaowafanya wajenge nyumba zao, kuoa au kuolewa na kufanya kazi.

Mchungaji Rwakatare ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 8, 2019 alipokuwa akitoa neno la uzinduzi wa Kongamano la 'Shilo 2019' lenye lengo la kuomba masuala mbalimbali kama amani ya Taifa na kuwaombea viongozi wa Tanzania akiwamo Rais wake, John Magufuli.

Ujumbe wa kwanza ambao kiongozi huyo wa kiroho ameutoa huku akishangiliwa na waumini wake, mwaka 2020 Mungu atawajaalia kila mmoja atajenga nyumba na kuhamia kwake ili kuepukana na adha ya kupanga.

 

“Nataka kuwapa ujumbe wa mwaka 2020, Mungu ametuambia jengeni majumba na mkakae ndani yake, hajasema pangeni, mnapanga kwa kujisaidia. Hajasema mkakae kwa kaka, mjomba au kwa nani, mnakaa kwa kujisaidia ila anasema jengeni nyumba mkakae ndani yake na kila mmoja anaweza kujenga,” amesema Mchungaji Rwakatare huku akishangiliwa.

Amesema umuhimu wa makazi hata Serikali ya Tanzania imetengeneza wizara, “na kumpa waziri mwenye hekima na busara, waziri wa muda , Willium Lukuvi ili akashughulikie.”

"Kama ulikuwa umejenga moja, kajenge nyingine, kila Mtanzania kajenge nyumba, siku hizi kuna viwanja hadi laki tano, siyo lazima kujenga Mikocheni, kajengeni hata Bagamoyo,” amesema.

Kuhusu ufanyaji kazi, amesema,” Pandeni mbegu kwenye mashamba yenu, mkale matunda yenu na mfanye kazi na asiyefanya kazi asile, Mtanzania fanya kazi, una nini cha kukuingizia kipato, unafanya kazi gani ikuingizie kipato, tufanye kazi na asiyefanya kazi na asile.”

Kiongozi huyo wa kiroho amezungumzia kuoa na kuolewa akisema, “Oeni wake mkazae watoto wa kike na wa kiume. Kawaozeni watoto na mpate wajukuu. Kama kuna Mtanzania mtu mzima oeni, wacha kunyemelea mke wa mwenzako, oeni mkazae."

Akishangiliwa na waumini kutoka nchi nzima waliokusanyika kwenye kongamano hilo la siku nane la maombi ya usiku na mchana, Mchungaji Rwakatare amesema, "Mwenye dada hakosi shemeji, oeni wake, mzae na kama hamjazaa Shilo ndilo suluhisho lake."

"Shilo ni wakati wa ukombozi, Shilo ni wakati wa ukombozi. Nasikia vilio vya watoto wachanga, wakilia ng'aa, ng'aa. Bwana Yesu apewe sifa na wakati wa Shilo ni wakati wa kufunga na kuomba."

Awali, Askofu Dunstan Maboyo alisema kupitia kongamano hilo, "Shilo ni maombi yenye dua, kila mmoja anapaswa kupata majibu kutokana na Shilo 2019. Shilo ikadumishe amani nchini Tanzania."

"Bendera yetu ya Tanzania inaakisi nchi ya kufanya kazi. Tulipata Uhuru bila kumwaga damu kwa hiyo tufanye kazi na kudumisha maombi."

Mmoja wa waumini, Ibrahim George amesema, “Imani bila matendo ni kazi bure kwa hiyo ujumbe wake una ukweli na kwa imani nyumba zitajengwa. Hili la kuona na kuolewa kama alivyosema kila mmoja aheshimu mke wa mwenzake."