VIDEO: Mdee, Bulaya hatihati kufutiwa dhamana

Muktasari:

Wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) kesho Jumanne 21,2020 wanatakiwa  kujieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kutoka nje ya Tanzania bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewataka wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) wajieleza kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kutoka nje ya Tanzania bila kibali cha Mahakama.

Pia. wadhamini wao wametakiwa kufika mahakamani hapo kesho Jumanne Januari 21, 2020 ili wajieleze kwa nini wasiondolewe kuwa wadhamini wa washtakiwa hao kwa kukiuka masharti ya udhamini.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliyasema hayo leo Jumatatu Januari 20, 2020 baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kueleza walipata taarifa kupitia vyombo vya dola kuwa Januari 19, 2020 washtakiwa hao walionekana wakiingia nchini kupitia usafiri wa Shirika la Ndege la Kenya.

Nchimbi akiwasilisha ombi hilo amedai washtakiwa  walipewa dhamana katika kesi hiyo pamoja na sharti mojawapo la kutosafiri nje ya Tanzania bila kupata kibali cha mahakama.

Hakuna ubishi kwamba walisafiri nje ya nchi, hoja ni je walipata kibali cha mahakama, Kwa maoni yangu walisafiri nje ya mahakama pasipokupata kibali cha mahakama.

"Katika maelezo ya Mdee mahakama iliandikiwa barua na hospitali ya Aga Khan ni rai ya upande wa mashtaka unapoomba ridhaa hatutegemei iombwe na hospitali kimsingi ilitakiwa iombwe na washtakiwa wenyewe," ameieleza Nchimbi.

Amebainisha mahakamani hapo kuwa Januari 13, 2020 alipokea barua iliyoandikwa na Wakili Hekima Mwasipu na wakapewa nakala na mahakama kwa busara Januari14, 2020 iliwaita upande zote ambapo ilikuwa ikiomba washtakiwa wote waende Kenya kwenye mkutano wa ndani na siyo Afrika Kusini na kwamba Januari 15, 2020 maombi hayo yalikataliwa.

Amesema sharti la kutokutoka nje ya nchi bila kibali cha mahakama lilikuwa ni sharti mahususi ni lazima washtakiwa waombe ruhusa

Wakili huyo amesema hilo alikufanyika, washtakiwa walikiuka dhamana hivyo kuomba wadhamini wao waitwe kujieleza kwa nini wasifutiwe udhamini wao kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Kwa upande wa washtakiwa nao wajieleze kwa nini wasifutiwe dhamana zao kwa kukiuka masharti ya dhamana .

Hata hivyo, wakati hayo yote yakiendelea John Mnyika ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema hakuwapo mahakamani hapo kwa sababu amefiwa na baba yake mdogo.

Mdhamini wake, Wilson Mosses ameieleza mahakama Mnyika alimpigia simu na kumpa taarifa kuwa amefiwa na baba yake mdogo Wilaya ya Misungwi Mwanza na kwamba mazishi yanafanyika Januari 20,2020 hivyo Jumatano atakuwa amekwisha rejea.

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Wemgine ni wabunge John Heche (Tarime Vijijini), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.

Katika kesi hiyo Mbowe na wenzake hao nane wanaokabiliwa na  mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi  makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.