Mdee, Bulaya na Matiko washindwa kutoka jela

Muktasari:

  • Wabunge watatu wa Chadema wameshindwa kutolewa leo Jumatano Machi 11, 2020 katika gereza la Segerea kwa kile kinachoelezwa kuwa mkuu wa gereza hilo kuwa na kikao.

 Dar es Salaam. Wabunge watatu wa Chadema wameshindwa kutolewa leo Jumatano Machi 11, 2020 katika gereza la Segerea kwa kile kinachoelezwa kuwa mkuu wa gereza hilo kuwa na kikao.

Wabunge hao ni Halima Mdee (Kawe), Ester Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya (Bunda).

Wabunge hao na wenzao watano akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walipelekwa gerezani jana kutokana na  kushindwa kulipa faini ya Sh320 milioni, baada mahakama  ya hakimu mkazi Kisutu kuwatia hatiani na kuwahukumu katika mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa wakiwakabili.

Wakili wa washtakiwa hao, Fred Khiwela ameiambia Mwananchi leo, Machi 11, 2020, saa 11:30 jioni kuwa tayari wameshakamilisha taratibu zote ikiwemo kulipa faini ya jumla ya Sh110 milioni kwa wabunge hao.

Khiwelo amesema kutokana na wateja wake kushindwa kutolewa leo, wamejipanga kesho asubuhi kuwatoa.

Mwananchi iliweka kambi karibu lango la kuingilia gerezani na kubaini  kuwa licha ya mkuu wa gereza kuwa na kikao, washtakiwa hao wameshindwa kutolewa kunatokana na wao kuchelewa kufika gerezani, hali iliyopeleka muda wa kazi kuisha.

Bulaya na Mdee walitiwa hatiani katika mashtaka manne kila mmoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh 40 milioni kila mmoja.

Kwa upande wake, Matiko alitiwa hatiani katika mashtaka matatu, hivyo kutakiwa kulipa faini ya Sh 30 milioni

Washtakiwa hao na wenzao walitiwa hatiani katika kesi ya uchochezi.