Mdude aeleza kilichomfanya asihamie Kenya

Mbeya/Dar. Mdude Nyagali, maarufu ‘Mdude Chadema’, amesema kutokana na misukosuko ambayo amekuwa akiipata alifikia hatua ya kutaka kuhama nchi ili akaishi uhamishoni, lakini alighaili akiwa njiani.

Mdude kwa sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuokotwa na madereva bodaboda kitongoji cha Mtakuja, Kijiji cha Inyala wilayani Mbeya.

Jumamosi ya Mei 4, Mdude, mkazi wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akiwa ofisini kwake mjini Vwawa, kisha akapelekwa kusikojulikana hadi alipokutwa usiku wa Jumatano iliyopita eneo la Inyala akiwa hoi kutokana na kipigo alichokipata.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo, Mdude alisema kutokana na misukosuko iliyokuwa inamkabili kabla ya tukio hilo aliomba msaada kwa viongozi wa Chadema na baadaye akazungumza na meya wa Ubungo, Boniface Jacob na mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ambao walimfanyia mpango kwenda kuishi nchini Kenya kabla ya kubadilisha uamuzi wake.

“Ni sahihi kabisa, kwani kuna kipindi misukosuko ilizidi, mara kesi mahakamani. Baadaye nikasema nitafute hifadhi nchi nyingine. Ndio wakawa wamenitafutia hifadhi Kenya, wakanifanyia michakato mingine yote. Na nikasafiri hadi Arusha kwa ajili ya kuelekea nchini Kenya,” alisema Mdude.

Alisema alipofika Arusha, nafsi yake ilimsuta, akafikiria kwamba akiondoka nchini watu wengi watakata tamaa, hivyo ni bora arudi kwa sababu Tanzania ni nchi yake.

Alisema uamuzi wake huo uliambatana na kumwachia Mungu kila jambo maishani mwake, na kama ana makosa basi atahukumiwa kwa makosa yake na iwapo yuko sahihi Muumba wake atamsimamia.

Jacob, Sungu

Akizungumzia uamuzi wa Mdude kutaka kutimkia uhamishoni, Meya Jacob alisema, “binafsi amenifundisha ujasiri, kuna wakati alikuwa anatumiwa meseji za vitisho na watu wasiojulikana, ilifikia hatua kama chama tukaona atafutiwe makazi nje ya nchi lakini yeye alikataa akasema ataendelea kuwepo hapa na kupambana hadi mwisho wake.”

Jacob, ambaye diwani wa Ubungo (Chadema), alisema kwa muda aliofahamiana na Mdude amemfundisha ujasiri na kutokata tamaa wala kukubali kuyumbishwa kifikra.

“Ni mpiganaji asiyekata tamaa, anasimama na kuonyesha wazi kupigania anachokiamini, haya matatizo si mara ya kwanza kumkuta na amekuwa akikutana na vitisho mara kadhaa, lakini hajawahi kuwa na hofu.”

Alisema umaarufu wa mwanachama huyo wa Chadema ambaye pia ni kiongozi wa mafunzo Kanda ya Nyasa umekuwa mkubwa kutokana na mwenendo wake wa kuikosoa Serikali kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Naye mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alimwelezea Mdude kuwa ni kijana mzalendo mwenye kusimamia kile anachokiamini na kutekwa kwake kunahusishwa na mwenendo wake wa ukosaji.

Alieleza kuwa mwanachama wao huyo amekuwa akiikosa Serikali kwa sababu anaamini ni nafasi yake ya kikatiba kama Mtanzania na vilevile ni kiongozi wa chama cha upinzani ambacho kina jukumu la kutoa mawazo mbadala ikiwemo kukosoa.

Uchunguzi wa polisi

Akizungumzia uchunguzi wa polisi, kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa Mdude, lakini wanapata ugumu kwa kuwa mhusika mwenyewe hasemi ukweli.

“Daah! Unauliza maswali magumu... Mdude mwenyewe hasemi waliomteka akina nani na kama yeye mwenyewe anasema hawajui, unafikiri sisi tutajua kweli? Anapaswa kusema gari lilikuwa na namba fulani, walioniteka walikuwa wanasema hiki, hiki na hiki, ili na sisi tuanzie hapo,” alisema kamanda Kyando.

“Tukimuuliza walipokuwa wanakupiga walikuwa wanakuambia nini? Hasemi. Sasa hapo tunafanyaje? Kimsingi majibu rahisi ni kwamba bado uchunguzi unaendelea, ukikamilika tutawaambia.”

Alisema, “Mdude hayupo wazi kwani lazima wanapokupiga wanasema kwa nini uliniibia au kwa nini ulifanya hivi au kwa nini umefanya hivi.”